PAZIA la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2016/17 limefungwa rasmi jana, huku Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, ikimaliza katika nafasi ya nne kwa pointi 52.

Azam FC imemaliza katika nafasi hiyo baada ya kupoteza mchezo wa mwisho wa ligi kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar jana, ukiwa ni ushindi wa kwanza wa timu hiyo kwenye Uwanja wa Azam Complex dhidi ya matajiri hao.

Hii ni mara ya kwanza kwa Azam FC kupoteza ndani ya uwanja wake wa nyumbani baada ya siku 938 kupita (sawa na miezi 30 na siku 25), tokea walipofungwa mara ya mwisho Oktoba 25, 2014 dhidi ya JKT Ruvu (1-0).

Kihistoria unakuwa ni mchezo wa tatu kupoteza ndani ya Azam Complex tokea uwanja huo uanze kutumika kwa mara ya kwanza Agosti 20, 2011 kwa Azam FC kuichapa Moro United bao 1-0, mechi zote zikiwa za Ligi Kuu, awali ikianza kufungwa na African Lyon bao 1-0 Agosti 23, 2011 kabla ya kufungwa tena na JKT baada ya miaka mitatu na ndani ya miaka mitatu mingine ikafungwa na Kagera Sugar jana.

Dondoo zingine zinaonyesha kuwa, Azam FC tokea msimu wa 2009/2010 iliposhika nafasi tatu, haijawahi kutoka kwenye tatu bora kwa misimu saba iliyopita, huku katika misimu hiyo ikimaliza ndani ya mbili bora kwa msimu mitano na kutwaa ubingwa mara moja (2013-2014).

Katika kuufunga msimu huo, Yanga imefanikiwa kuwa mabingwa kwa kutetea ubingwa wao kwa pointi 68 sawa na Simba iliyokamata ya pili na Kagera Sugar imemaliza katika nafasi ya tatu ikifikisha 53 ikiizidi pointi moja Azam FC.

Timu tatu zilizoshuka daraja kuzipisha Singida United (Singida), Njombe Mji (Njombe) na Lipuli (Iringa) zilizopanda daraja kwa ajili ya msimu ujao ni JKT Ruvu iliyomaliza mkiani kwa pointi 23, Toto African (29) na African Lyon (32).

Wakati Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting, akiibuka mfungaji bora wa msimu kwa mabao 14 aliyofunga sawa na Simon Msuva wa Yanga, nahodha wa Azam FC John Bocco ‘Adebayor’, ndiye kinara wa ufungaji bora Azam FC licha kukosa mechi nyingi msimu huu kutokana na majeraha, akifunga tisa VPL na 12 kwenye mashindano yote.

Kikosi cha Azam FC jana:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Bruce Kangwa, Agrey Morris, Yakubu Mohamed/Khamis Mcha dk 46, Daniel Amoah, Stephan Kingue, Himid Mao (C)/Mudathir Yahya dk 72, Salum Abubakar, Ramadhan Singano, Shaaban Idd