KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kufanya ziara maalumu ya siku tano mkoani Arusha ikitarajiwa kuelekea huko Mei 24 na kurejea Mei 29 jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo inatokana na mwaliko maalum waliopata kutoka Shule ya Trust St. Patrick, iliyopo maeneo ya Sakina mkoani humo, ambayo pia imesajiliwa kama kituo cha michezo.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, alisema kuwa ziara hiyo itaambatana na mechi mbili za kirafiki zitakazotangazwa hapo baadaye pamoja na kuwapa pole wafiwa kufuatia ajali ya basi iliyotokea hivi karibuni iliyohusisha wanafunzi wa Shule ya Lucky Vincent.

“Tumealikwa na wenyeji wetu Arusha, watatugharamia kila kitu wao wametaka Azam FC iende kwa sababu muda mrefu hawajaiona na mashabiki wanahitaji kuiona, sisi tumeona tusiwanyime nafasi hii kwani wenzetu wapo kwenye kipindi kigumu sasa hivi hivyo wanahitaji kupata angalau burudani ndogo kuwaondoa kidogo katika majonzi waliyokuwa nayo,” alisema.

Huu ni mwendelezo mzuri wa Azam FC kuungana na jamii katika vipindi vya huzuni, itakumbukwa kuwa Novemba mwaka jana timu hiyo ilikwenda kuwapa pole waathirika wa tetemeko ardhi mjini Bukoba, mkoani Kagera, wakati ilipokwenda kupambana na Kagera Sugar na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.

St. Patrick wanasemaje?

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Trust St. Patrick School, Dinnah Patrick, alisema wameamua kuichagua Azam FC ili kujenga mahusiano kutokana na timu hiyo kuwa na uzoefu wa kutosha kwenye nyanja hiyo ya michezo.

“Tunachohitaji kutoka Azam FC kikubwa ni kujifunza, kwa sababu kituo cha Azam kimeanza muda mrefu na kwa sababu kituo chetu kama tulivyosema kina mwaka mmoja na miezi miwili, basi ni vizuri kujua wadau wenzako wanafanyaje, ambao mnaweza kubadilishana mambo mbalimbali,” alisema.

Historia fupi ya St. Patrick

Shule hiyo ilianza mwaka 1997 kama shule ya awali na msingi, na pia ikafungua wigo kwa kuanzisha shule ya sekondari mwaka 2006 kwa wavula pekee.

Baada ya mafanikio, wakuu wa shule hiyo waliamua kuisajili timu hiyo kama kituo cha michezo mwaka jana, kikihusisha michezo mbalimbali ikiwemo riadha, mpira wa kikapu, mikono, tenesi na mpira wa miguu huku wakiwa na miundombinu ya kuchezea michezo hiyo.

Katika mipango waliyojiwekea ambayo wameanza kuifanyia kazi ni kukifanya kituo hicho kuwa kikubwa na kujenga uwanja mkubwa wa soka wenye sehemu za kukimbilia riadha, utakaobeba watu wasiopungua 16,000, pamoja na hoteli na hosteli pembezoni mwa uwanja huo.