KESHOKUTWA Jumamosi, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itafunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kukipiga dhidi Kagera Sugar katika Uwanja wa Azam Complex, saa 10.00 jioni.

Mchezo huo unatarajia kuwa na ushindani mkali kwa pande zote mbili, hasa ikizingatiwa timu hizo zinawania kumaliza ligi kwenye nafasi ya tatu, ambapo kwa sasa zinapishana pointi mbili tu, Azam FC ikishika nafasi hiyo baada ya kufikisha 52, huku Kagera Sugar ikiwa nazo 50.

Wakati timu hizo zikienda kupambana, huenda hii ikawa ni habari mbaya kwa upande wa Kagera Sugar, kwani inakwenda kukipiga ndani ya dimba la Azam Complex, ikiwa na rekodi mbaya zaidi ya kutowahi kuambulia sare au ushindi kwenye uwanja huo dhidi ya Azam FC.

Azam FC imeonekana kuwa kiboko ya Kagera Sugar kwa kufanikiwa kuzoa pointi zote 15 katika mechi tano walizokutana kwenye ligi ndani ya uwanja huo, huku katika mabao yote 16 yaliyowekwa kimiani, matajiri hao wakitupia nyavuni 13 na Kagera ikiziona nyavu za Azam Complex mara tatu tu.

Ni mechi tatu ambazo Azam FC ilikuwa nyumbani na imecheza nje ya Azam Complex kutokana na kutokukamilika kwa uwanja wake, kati hizo imefanikiwa kuvuna pointi moja tu kufuatia sare na kupoteza miwili iliyobakia.

Rekodi kamili inaonyesha kuwa kihistoria timu hizo zimekutana mara 17 kwenye mechi za ligi, Azam FC ikishinda mechi tisa kati ya hizo, sare nne na kupoteza mechi nne.

Katika mechi sita zilizopita dhidi ya Kagera Sugar, iwe nyumbani au ugenini Azam FC imefanikiwa kushinda michezo yote ikivuna jumla ya pointi 18, jambo ambalo linaipa nafasi nzuri zaidi ya kuibuka kidedea kwenye mchezo ujao wa Jumamosi na kumaliza nafasi ya tatu.

Katika mchezo huo, Azam FC itanufaika na urejeo wa viungo wake wawili, Himid Mao ‘Ninja’ na Stephan Kingue, walioukosa mchezo uliopita, huku ikimkosa nahodha wake John Bocco ‘Adebayor’, ambaye amekusanya kadi tatu za njano na kiungo Frank Domayo ‘Chumvi’, ambaye bado anasumbuliwa na nyama za paja.

Ushindi wowote wa Azam FC, utaifanya kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu na kufikisha jumla ya pointi 55.

Mechi zote walizocheza VPL     

28/10/16       Kagera Sugar  2 – 3  Azam FC (W)

08/05/16             Kagera Sugar  1 – 2  Azam FC      (W)

27/12/15       Azam FC  2 – 0   Kagera Sugar (W)

18/04/15       Azam FC  2 – 1   Kagera Sugar (W)

20/01/15       Kagera Sugar 1 – 3  Azam FC       (W)

02/02/14     Azam FC   4 – 0   Kagera Sugar (W)   

14/09/13      Kagera Sugar   1 – 1   Azam FC (D)

26/01/13      Azam FC  3 – 1  Kagera Sugar      (W)

15/09/12             Kagera Sugar   0 – 1   Azam FC (W)

06/05/12      Azam FC   2 – 1   Kagera Sugar (W)

30/10/11             Kagera Sugar   0 – 0   Azam FC (D)

15/01/11      Azam FC   1 – 2   Kagera Sugar  (L)

15/09/10       Kagera Sugar   1 – 0   Azam FC  (L)   

18/01/10      Azam FC   1 – 1   Kagera Sugar  (D)   

23/08/09      Kagera Sugar   3 – 2   Azam FC  (L)

14/04/09       Kagera Sugar   1 – 1   Azam FC  (D)

18/10/08       Azam FC   1 – 2   Kagera Sugar (L)

 

*Azam FC: Win : 9, Draw : 4, Lose : 4