KIPA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aishi Manula, ni miongoni mwa nyota watano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) waliochaguliwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa ligi hiyo msimu huu.

Wachezaji wengine wanaowania tuzo hiyo ni kiungo Haruna Niyonzima na winga Simon Msuva kutoka Yanga pamoja na winga Shiza Kichuya na beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inaeleza kuwa wapiga kura watakaohusika kumchagua mchezaji bora ni makocha wakuu na wasaidizi na manahodha wa timu za Ligi Kuu pamoja na wahariri wa michezo kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Wakati zoezi la kupiga kura likitarajiwa kufika tamati Mei 23 mwaka huu saa 6.00 usiku, wahusika wote watakaopiga kura hizo watatumiwa fomu maalum za kupiga kura kwenye barua pepe za klabu na vyombo husika vya habari.

Hafla ya utoaji tuzo hiyo, ambayo inaratibiwa na Kamati ya Ushauri ya Rais wa TFF itafanyika Mei 24 mwaka huu kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Rekodi za Manula (VPL, 2016-2017)

Manula anachaguliwa kuwania tuzo hiyo baada ya kufanikiwa kuwa kwenye kiwango kizuri, mpaka sasa ligi ikielekea kumaliza mchezo wa raundi ya mwisho wikiendi hii, kipa huyo amefanikiwa kudaka mechi 28 (sawa na dakika 2,520) kati ya 29 zilizochezwa hadi sasa.

Katika mechi hizo 28, Manula ambaye ni mmoja wa makipa tegemeo wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, efanikiwa kuiongoza Azam FC kutoruhusu wavu wake kuguswa katika mechi 15 na ni 13 tu alizoruhusu kufungwa, ikiwa ni rekodi nzuri kuliko kipa mwingine yoyote ndani ya ligi hiyo msimu huu.

Mechi moja ambayo ameikosa Manula msimu huu ni ile dhidi ya Mbao, iliyofanyika kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na Azam FC iliteleza kwa kufungwa mabao 2-1.

Itakumbukwa kuwa, kipa huyo aliyekulia kwenye kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC ‘Azam Academy’ kabla ya kupandishwa misimu mitatu iliyopita, anashikilia tuzo mbili za kipa bora alizopata msimu uliopita, akitwaa ya kipa bora wa Ligi Kuu pamoja na ile ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).