KAZI Haijaisha! Hiyo ndio kauli aliyotoa Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa jana dhidi ya Toto African, amedai kuwa bado kuichapa Kagera Sugar katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi ijayo.

Azam FC iyoibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Toto kwa mabao safi yaliyofungwa na Shaaban Idd na Ramadhan Singano ‘Messi’, ipo kwenye na vita na Kagera Sugar ya kuwania nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, matajiri hao wakiwa wameshikilia nafasi hiyo wakiwa na pointi 52 huku Kagera Sugar yenye michezo miwili mkononi ikiwa nazo 47.

Cioaba ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa kikosi chake kinazidi kuimarika kadiri siku zinavyosonga mbele huku akijiamini kwa kusema kuwa Azam FC itakuwa ni timu bora na tishio msimu ujao.

“Tunamshukuru Mungu kwa kukusanya pointi tatu nyingine baada ya wiki iliyopita kuifunga Mbao, tumekuwa tukicheza soka zuri kadiri siku zinavyokwenda, hakika wachezaji wangu wamefanya kazi kubwa na wanazidi kuimarika kila siku, licha ya kuwakosa wachezaji muhimu kwenye eneo la kiungo lakini tuliweza kucheza vema na kupata kile tulichohitaji,” alisema.

Mromania huyo alizungumzia viwango vizuri vinavyoendelea kuonyeshwa na Singano na Shaaban, akisema kuwa: “Nafarijika kuwaona wachezaji wangu vijana Shaaban na Singano wakiendelea kuongezeka viwango kwenye mechi hadi mechi, hii ni ishara nzuri kwako na kwa timu, wamekuwa wakifanya kazi nzuri mazoezini na kwenye mechi wamekuwa msaada kwa timu, nina imani watakuwa vizuri zaidi msimu ujao pamoja na wachezaji wengine.”

Kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana, alisema kuwa bado kazi haijaisha msimu huu kwani wanatakiwa kuifunga Kagera Sugar katika mchezo wa mwisho wa ligi ili kusalia kwenye nafasi ya tatu katika ligi.

Kuelekea mchezo huo wa mwisho wa ligi, Azam FC itaaanza rasmi maandalizi Jumatatu ijayo jioni na itakumbukwa kuwa katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, matajiri hao walishinda 3-2, mabao ya Azam FC yakifungwa na nyota wake Mudathir Yahya, Frank Domayo na Nahodha John Bocco’Adebayor’ akitupia la ushindi.