KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imezidi kufanya kweli baada ya kuichapa Toto African ma bao 2-0, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliomalizika usiku huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Walikuwa ni Shaaban Idd na Ramadhan Singano ‘Messi’, waliopeleka kilio kwa Toto African baada ya kuifungia Azam FC mabao hayo pekee katika mchezo huo wa raundi ya 29 ya ligi hiyo.

Wakati ushindi huo ukizidi kuipa matumaini makubwa Azam FC kumaliza katika nafasi ya tatu ya ligi baada ya kufikisha jumla ya pointi 52, kwa upande wa Toto hali imezidi kuwa mbaya kwa upande wao, ambapo kwa sasa wanahitaji kushinda mechi zao mbili zilizobakia kwenye ligi ili kuepuka janga la kushuka daraja.

Katika mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, aliendelea na mfumo wake wa 3-4-3, akiwatumia mabeki watatu wa kati, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed na Daniel Amoah, mfumo ambao umeonekana kufanya vema tokea alipoanza kuutumia.

Lakini Mromania huyo aliwakosa wachezaji wake muhimu wa kikosi cha kwanza kwenye eneo la kiungo, nahodha msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, ambaye bado hajarejea nchini baada ya kuwa kwenye majaribio katika timu ya Randers ya nchini Denmark, Frank Domayo mwenye maumivu ya nyama za nyuma ya paja na Stephan Kingue, aliyekuwa akitumikia adhabu ya kukusanya kadi tatu za njano.

Iliichukua dakika 12 tu, Azam FC kuweza kuandika bao la uongozi lililofungwa kwa kichwa safi na Shaaban Idd, aliyeunganisha krosi nzuri ya beki wa kushoto Bruce Kangwa, bao lilomfanya kufikisha jumla ya mabao saba kwenye chati ya ufungaji bora msimu huu.

Kinda huyo alijikuta akikosa bao jingine la wazi dakika mbili baadaye baada ya kuiparaza kwa mguu wake krosi safi nyingine iliyochongwa na Kangwa, na hivyo kufanya mtanange huo umalizike kipindi cha kwanza kwa uongozi wa bao hilo.

Azam FC iliyofanikiwa kumiliki mchezo huo kwa kiasi kikubwa, iliweza kuongeza kasi ya mashambulizi kipindi cha pili na katika dakika ya 46, beki wa kulia Shomari Kapombe, aliwatoka mabeki wa Toto na kupiga shuti lililopanguliwa na kipa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Jitihada za Kapombe za kutaka kuipatia bao jingine Azam FC ziliweza kuzaa matunda dakika ya 50 baada ya kuipenya ngome ya ulinzi ya Toto na kutoa pande safi kwa Singano, ambaye alikutana na mpira huo uliokuwa ukielekea kutoka na kuutumbukiza wavuni na kuiandikia bao la pili mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu.

Matajiri hao wa Azam Complex, walizidi kulisakama lango la wapinzani wao ili kutaka kupata mabao zaidi, lakini nguvu kubwa walizokuwa wakizitumia kwa nyakati fulani ziliweza kuzimwa na mwamuzi wa mchezo huo, Shakaile Ole Yangalai kutoka mkoani Arusha, ambaye kwa kiasi kikubwa alishindwa kutafsiri sheria 17 za mchezo wa soka.

Huo ni ushindi wa sita kwa Azam FC dhidi ya Toto African kwenye mechi 12 za ligi walizokutana tokea msimu wa 2009/10, huku Toto ikiwa imeshinda mara moja tu na mechi tano wakienda sare, jumla ya mabao 34 yamefungwa (Azam FC 24, Toto 10).

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitakuwa na mapumziko ya siku mbili kabla ya kuanza rasmi mazoezi Jumatatu ijayo jioni kujiandaa na mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Kagera Sugar, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Mei 20, mwaka huu saa 10.00 jioni.

Mechi hiyo itafanyika jioni kutokana na michezo yote ya mwisho ya ligi kufanyika muda mmoja, ili kukwepa upangaji matokeo.

Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Bruce Kangwa, Daniel Amoah, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Shaaban Idd/Khamis Mcha dk 70, Salum Abubakar, John Bocco (C)/Gadiel Michael dk 90+2, Ramadhan Singano/Masoud Abdallah dk 86