ZIMEBAKIA saa kadhaa kabla ya kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, hakijashuka dimbani kuvaana na Toto African ya mkoani Mwanza, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaokuwa na vita kuu mbili baina ya timu hizo.

Vita hizo ni ile ya Azam FC ambayo itakuwa ikisaka pointi tatu muhimu kwa ajili ya kujikita katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, huku ile ya pili ikiwa ni ya Toto ambayo inasaka ushindi ili kujinasua kwenye janga la kushuka daraja.

Azam FC ipo katika nafasi hiyo baada ya kujisanyia jumla ya pointi 49 ikiizidi Kagera Sugar inayoifukuzia kwa karibu ikiwa nazo 47, Toto inayowania nafasi ya kubaki Ligi Kuu ipo kwenye nafasi tatu za mkiani (14) baada ya kujikusanyia pointi 29 na inatakiwa kushinda mechi zote mbili zilizobakia ili kujinasua katika mtego huo.

Kikosi cha Azam FC kwa wiki yote hii kimekuwa kwenye maandalizi makali chini ya Kocha Mkuu Aristica Cioaba, licha ya mvua zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo mengi nchini, yote hayo ni kuhakikisha inashinda mechi zote mbili ilizobakiza na kumaliza ligi katika nafasi tatu za juu.

Kuelekea mchezo huo, mtaalamu huyo Cioaba amesema kuwa kikosi chake kipo vizuri na wachezaji wake wapo tayari kwa mapambano ya kuwania pointi tatu muhimu, huku akiwaomba mashabiki wa Azam FC kujitokeza kwa wingi kuiunga mkoano timu hiyo kwa kuishangilia.

Cioaba hakusita kuweka wazi kuwa atawakosa wachezaji wake watatu muhimu kwenye eneo la kiungo, nahodha msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, ambaye bado hajarejea nchini baada ya kuwa kwenye majaribio katika timu ya Randers ya nchini Denmark, Frank Domayo, anayesumbuliwa na maumivu ya nyama za nyuma ya paja.

Aidha kiungo Stephan Kingue, naye atakosekana kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano baada ya kupata kadi ya tatu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mbao, ulioisha kwa Azam FC kuichakaza timu hiyo kwa mabao 3-1.

Takwimu zinasemaje?

Kwa mujibu wa takwimu tokea timu hizo zilipoanza kukutana kwa mara ya kwanza kwenye msimu wa 2009/10, zinaonyesha wamekutana mara 11 kwenye ligi, Azam FC ikiwa imeshinda mara tano, imepoteza mmoja na timu hizo kwenda sare mara tano.

Jumla ya mabao 32 yamefungwa baina ya timu zote mbili kwenye mechi hizo, Azam FC ikiwa imefunga robo tatu ya mabao yote yaani 22 huku toto African ikifunga 10 pekee.

Katika mchezo wa kwanza msimu huu uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Azam FC iliibuka na ushindi wa 1-0 lililofungwa na Shaaban Idd aliyepokea pande safi kutoka kwa nahodha John Bocco ‘Adebayor’, na timu hiyo kuandika historia ya kushinda mchezo wa kwanza ndani ya uwanja huo.

Itakumbukwa kuwa mara ya mwisho Toto African kukanyaga kwenye ardhi ya Azam Complex, iliweza kukumbana na kipigo kizito kutoka kwa matajiri hao baada ya kukubali kufungwa mabao 5-0 mchezo uliofanyika msimu uliopita Novemba Mosi, mwaka juzi.

Mabao ya Azam FC yaliwekwa kimiani na beki Shomari Kapombe, aliyepia mawili mawili sawa na mshambuliaji nyota wa zamani wa timu hiyo, Didier Kavumbagu na straika mwingine hatari, Kipre Tchetche aliyeingia wavuni mara moja. 

Hivyo wataingia dimbani wakiwa na kumbukumbu ya kukutana na kisago hicho ndani ya uwanja huo, huku pia wakiwa na mtihani mzito wa kusaka ushindi ili kujinasua mkiani.