IKIWA inamalizia maandalizi yake ya mwisho leo jioni kabla ya kuikabili Mbao kesho Jumamosi, habari njema ni kuwa kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kipo tayari kabisa kuivaa timu hiyo.

Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), utafanyika katika Uwanja wa Azam Complex, saa 1.00 usiku, ambapo Azam FC itakuwa ikisaka ushindi ili kuendelea na vita ya kubakia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa kwanza, ulioisha kwa Mbao kushinda mabao 2-1, bao pekee la mabingwa hao likifungwa na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Francisco Zekumbawira, aliyepokea pasi safi ya nahodha John Bocco ‘Adebayor’.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alisema vijana wake wako vizuri mazoezi jambo ambalo linampa matumaini ya kuibuka na ushindi katika mtanange huo unaotarajia kuwa mkali.

“Kikosi changu kipo vizuri kuelekea mechi tatu za mwisho za kumaliza ligi, isipokuwa Himid Mao ambaye hayupo kikosini akiwa majaribioni Denmark, mechi zote hizi ni muhimu kwa kikosi changu na jambo zuri wachezaji wanaonyesha ari nzuri mazoezini.

“Nimejaribu kuwaambia wasahau yaliyopita kwenye mchezo wa FA Cup kwani kila mtu amejionea mambo yasiyo ya kimpira yaliyotokea, na kikubwa waweke akili yao katika mechi zinazokuja, ikianzia na hii ya kesho dhidi ya Mbao, ambayo ni muhimu kushinda na ninachoahidi kwa mashabiki ni kuonyesha mchezo mzuri na kuibuka na ushindi,” alisema.

Azam FC yenye udhamini wa Benki bora kabisa nchini ya NMB na kinywaji safi na burudani kwa mwili wako cha Azam Cola, kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 46 sawa na Kagera Sugar, yenye mchezo mmoja mkononi, ambapo ushindi wa mechi zote zilizobakia utaifanya kumaliza katika nafasi ya tatu.