GUMZO kubwa hivi sasa linaloendelea kwenye mitandao ya kijamii kwenye anga ya soka nchini, ni uchezeshaji mbovu uliokithiri wa mwamuzi wa kati, Metthew Akrama, katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) kati ya Simba na Azam FC.

Uamuzi wake mbovu uliozua utata kwa kiasi kikubwa ulionekana kuiathiri Azam FC na kupelekea Simba kutinga fainali ya michuano hiyo na sasa ikitarajiwa kucheza na Mbao, ambayo nayo imepata ushindi kama huo leo dhidi ya Yanga.

Mwamuzi huyo Akrama, mwenye historia ya kutoa kadi nyekundu na kuchezesha hovyo kwenye mechi za timu hiyo alitimiza kile alichokipanga na kuonekana kufuata maelekezo aliyopewa, kwa kuamua kumpa kadi nyekundu yenye utata kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dakika ya 15.

Kitendo hicho cha Azam FC kucheza pungufu kwa muda mrefu wa mchezo huo kwa kadi isiyostahili, kiliharibu mipango ya timu hiyo na hatimaye Simba ikanufaika na kupata kile walichoandaliwa na wakubwa wa soka.

Mwaka 2011, Akrama aliwahi kumpa kadi nyekundu nahodha John Bocco ‘Adebayor’, kwenye pambano dhidi ya Simba lililofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Azam FC kufungwa 2-1 katika ligi huku akikataa bao kiungo wa zamani wa timu hiyo, Ramadhan Chombo ‘Redondo’.

Mbali na jana Azam FC kupata kadi hiyo, pia mwamuzi huyo aliinyima penalti za wazi timu hiyo ikiwemo ile ya beki Juuko Murshid, aliyezuia mpira kwa mkono hadharani, lakini kutokana na waamuzi kufuata maelekezo waliamua kulifumbia macho tukio hilo.

Azam FC kuwa na rekodi nzuri dhidi ya Simba msimu huu, ikishinda mechi mbili mfululizo zilizopita ni moja ya mambo yaliyopelekea waamuzi hao kuziweka pembeni sheria 17 za mchezo wa soka, na kutimiza kile walichotumwa na wakubwa.

Hivyo kilichotengenezwa ili kuamua mchezo huo na kupatikana kile kilichotakiwa na wakubwa hao, ilikuwa ni kutafuta namna ya kuidhoofisha kivyovyote Azam FC mchezoni ili ipoteze mtanange huo na Simba kuingia fainali kama ilivyopangwa.

Haikushangaza kuona vitendo vya ushirikina vikifanywa waziwazi na mtu anayesadika kuwa ni wa Simba ndani ya uwanja kabla ya mchezo huo, lakini cha kushangaza alichukuliwa na polisi na baadaye watu walipambana na mtu huyo kuachiwa.

Vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina vimeainishwa na kupingwa vikali kwenye kanuni za Ligi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini cha kushangaza mpaka sasa shirikisho hilo lipo kimya, na hiyo inadhihirisha ya kuwa wamekubaliana na yote yaliyofanyika katika mchezo huo wa jana.

Itakumbukwa kuwa Simba imefika hapa baada ya sheria za michuano hiyo kupindishwa kwa timu ya Polisi Dar es Salaam kunyimwa haki yake na TFF ya kuingia hatua ya 16 bora baada ya wekundu hao kukiuka kanuni ya kumjumuisha kikosini mchezaji mwenye kadi nyekundu, beki Novart Lufunga, aliyopata katika mechi yao ya mwisho ya msimu uliopita dhidi ya Coastal Union.

Kupita kwa Simba isivyo kihalali na timu nyingine kunyimwa haki yake, ni moja ya mambo yanayozidi kudhihirisha namna TFF ilivyokuwa ikipambana kuiona timu hiyo ikifika mbali kwenye michuano hiyo na kunufaika na kile walichokuwa na maslahi nacho.

Dunia hivi sasa ni kijiji na kwa hakika nchi jirani zinazoshuhudia mechi zetu moja kwa moja kupitia Azam TV na hata wageni wanaokuwa wamekuja kutafuta malisho kwenye vilabu vyetu hapa nchini, wamekuwa wakishangazwa sana na namna soka letu linavyotafunwa na siasa pamoja na waamuzi ambao wamekuwa wakichezesha kwa maelekezo.

Kila kukicha tumekuwa wagumu kukubaliana na neno ‘fair play’ yaani mchezo wa kiungwana, ambalo limesisitizwa pia kwenye kanuni za TFF, mbali na wachezaji kufanyiana haki uwanjani, pia kanuni hizo zinasisitiza kupatikana matokeo ya haki.

Nanukuu Kanuni ya 24 ya Ligi;

Uchezaji wa Kiungwana (Fair Play)

Wachezaji wanatakiwa kuzingatia kanuni za mchezo wa kiungwana ‘fair play’ ndani na nje ya uwanja wa mchezo. Kanuni 10 za FIFA za mchezo wa kiungwana ni kama ifuatavyo:

i) Cheza Kiungwana – Ushindi hauwezi kuwa na thamani iwapo umepatikana katika njia isiyo halali au kwa udanganyifu. Kudanganya ni rahisi lakini haileti raha ya ushindi. Kucheza kiungwana inahitaji moyo na tabia njema. Pia hufurahisha zaidi. Mchezo wa kiungwana siku zote una malipo yake hata kama utapoteza mchezo. Kucheza kiungwana kunakujengea heshima wakati kudanganya kunaleta aibu. Kumbuka kuwa mpira wa miguu ni mchezo na mchezo wowote hauwezi kuwa na maana kama hautochezwa kiungwana kwa kuzingatia kanuni na taratibu ili mshindi halali aweze kupatikana.

Inashangaza Kanuni tumeziweka wenyewe, lakini mwisho wa siku tunashindwa kuendana nazo na kujiamulia cha kufanya nje ya kanuni za soka kwa manufaa binafsi, ambayo hayalisaidii soka letu.

Tumebakia kwenye sayari ya peke yetu, kila kukicha mipango ya kulitafuna soka letu na ndio maana tunashindwa kupiga hatua na haishangazi kutuona tukiwa kwenye nambari 135 kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), yaani tukiwa tumeachwa mbali na Uganda, Kenya na Rwanda, ambao wameacha misingi ya soka la kizamani la siasa ya kuzibeba baadhi ya timu na kuruhusu ‘fair competition’.

TFF inaposhindwa kuruhusu ushindani wa haki ‘fair competition’ kwenye mechi za mashindano hapa nchini, dhambi hii itaendelea kulitafuna soka letu kila siku yaani badala ya kupiga hatua, sisi tutaendelea kushuka kila siku na hatimaye Somalia, visiwa vya Comoro na mataifa mengine machanga yatatuacha kwenye mataa.

Tumekuwa na ligi isiyokuwa na weledi kwenye vyombo vya usimamizi, imekuwa ni kawaida kwa msimu wa pili mfululizo kutokea tukio la mchezaji kuhusishwa kucheza akiwa na kadi ya tatu ya njano na hii imetokea katika vipindi ambavyo ligi inaelekea mwishoni kwenye kuamua bingwa na timu gani zinazofuatia.

Msimu uliopita, tuliona namna Azam FC ilivyopokwa pointi tatu kwa Bodi ya Ligi kudai ilimchezesha beki Erasto Nyoni, akiwa na kadi tatu za njano kwenye mchezo wa Februari 20, 2016 dhidi ya Mbeya City.

Nyoni alidaiwa kukusanya kadi hizo kwenye Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Tanzania Prisons na Coastal Union, jambo ambalo lilishindwa kuwa na uhalali wa moja kwa moja kutokana na mapitio ya mikanda ya televisheni ya mchezo wa Azam FC dhidi ya Prisons, kutoonyesha tukio lolote na beki huyo kupewa kadi ya njano, lakini matajiri hao wakapokwa haki yao.

Msimu huu tukio kama hilo liliiangukia Kagera Sugar kwa mchezaji wao Mohamed Fakhi, kudaiwa alicheza akiwa na kadi tatu za njano kwenye mchezo dhidi ya Simba iliyokuwa inawania ubingwa, ambao walishinda 2-0 na kuiweka kwenye wakati mgumu timu hiyo.

Hatimaye ilishuhudiwa Kagera ikipokwa pointi tatu na kupewa Simba na Kamati ya Saa 72, lakini kutokana na Yanga ambayo nayo ina maslahi na ubingwa kushupalia suala hilo kupinga uonevu uliofanyika, hatimaye pointi tatu zilirejeshwa kwa wenye haki Kagera Sugar na Kamati ya Rufani ya TFF.

Haya matukio yanaibuka sana hivi sasa kutokana na wahusika kutokuwa na uweledi kwa kutimiza kile wanachokitaka; Bodi ya Ligia ma TFF wanashindwaje kutumia mfumo wa wenzetu waliopiga hatua wa kuzikumbusha klabu wachezaji wasiostahili kucheza mchezo husika kutokana na kadi?.

Inasikitisha sana kuona soka letu likichezewa na wachache, na kupoteza mamilioni ya pesa yanayotumiwa na timu kwenye mambo yake mbalimbali ya uendeshaji wake kama kulipa mishahara, maandalizi ya mechi na pesa za safari, lakini hakuna anayejali na mwishowe ubabaishaji kuendelea kila kukicha kwa timu zisizo na sauti kuonewa.

Bodi ya Ligi ambayo inatakiwa kulinda maslahi ya vilabu vyote, nayo imekuwa ikiingia kwenye aina hiyo ya upendeleo wa baadhi ya timu kwenye maamuzi na hatimaye klabu mbili pekee kupewa kipaumbele kila kukicha.   

Wenye mamlaka ya soka wanatumia nguvu kubwa sana kupambana kwenye masuala yasiyolisaidia soka letu, kuliko kufuata njia sahihi za kuliondoa ICU soka letu, huu ni udhaifu mkubwa na unaliweka kwenye aibu kubwa soka letu na ipo siku moja tutakuja kuumbuka vibaya kwani dunia hivi sasa ni kujiji na kila kitu kinaonekana hadharani.

Hili ndio soka letu tumejifungia kwenye kijiji chetu kisichopiga hatua, tunafanya tunavyotaka na hakuna wa kutuuliza. Tukitaka fulani awe bingwa atakuwa tu na tukitaka kuizua timu fulani tusiyokuwa na maslahi nayo tutaweza kulitimiza hilo kwa njia yoyote ile.  

Je, uonevu huu utaisha lini ikiwemo suala la kuwapa maelekezo waamuzi? Na tunafanya haya kwa faida gani kwenye soka letu? Wasimamizi wa soka letu wanapaswa kujitahimini na kisha wachukue hatua, la sivyo kila siku itakuwa ni afadhali ya jana.