WADHAMINI wakuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Benki ya NMB leo ilifanya ziara katika makao makuu ya timu hiyo ‘Azam Complex’.

Ziara hiyo ilikuwa na malengo makuu mawili, la kwanza ilikuwa ni kuwakutanisha mashabiki wa timu hiyo na wachezaji nyota wa kikosi hicho, nahodha msaidizi Himid Mao ‘Ninja, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na beki kisiki Shomari Kapombe.

Wachezaji hao walipata fursa ya kujibu maswali ya mashabiki kwenye zoezi ambalo lilikuwa likiruka mubashara kwenye akaunti ya facebook ya ukurasa wa benki hiyo ‘NMB PLC Tanzania’ na ule wa Azam FC.

Zoezi hilo la kuwaunganisha mashabiki na wachezaji ni la kwanza kuwahi kufanywa na klabu nchini, ambalo lilikuwa la kuvutia kutokana na vionjo mbalimbali na namna nyota hao walivyokuwa wakijibu maswali.

Mara baada ya kumalizika kwa mahojiano hayo, wafanyakazi wa benki hiyo kupitia timu yao ya mpira wa mguu ilipata fursa ya kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya vijana wenye umri wa miaka 20 ‘U-20’ ya Azam FC, iliyoisha kwa NMB kukubali kwa taabu kichapo cha mabao 7-3, huku ikishuhudiwa wakikosa penalti mbili.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa aina yake sambamba na kuburudisha kutokana na ufundi uliokuwa ukionyeshwa na timu zote uwanjani na watu waliokuwa wakishuhudia kila mara walikuwa wakiinuka vitini na kushangilia.

Benki ya NMB inayoongoza kwa sasa nchini ikiwa na matawi mengi yaliyosambaa nchini kote, imekuwa na ushirikiano mkubwa wa udhamini na Azam FC kwa msimu wa tatu mfululizo tokea msimu wa 2014/2015.