HAWACHOMOKI! Ndio unavyoweza kuitafsiri hivyo kauli ya Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, ambaye ametamba kuwa amekiandaa kikosi chake kupata matokeo mazuri dhidi ya Simba, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) utakaofanyika Uwanja wa Taifa kesho Jumamosi saa 10.00 jioni.

Azam FC imemaliza maandalizi yake kuelekea mchezo huo na ushindi wowote kesho utakuwa ukiifanya kuingia fainali na kutanguliza mguu mmoja kwenye kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Cioaba amesema kuwa mbali na mchezo huo kuwa mgumu amekipanga kikosi kupata matokeo mazuri huku akifurahishwa na morali kubwa anayoiona kikosini.

“Nilianza maandalizi ya mchezo huu Jumatatu na wachezaji, hivi sasa ni wiki moja kila mchezaji ni mzuri ndani ya mazoezi nina furaha kubwa kuwa wachezaji wapo tayari kwa mchezo huo na naahidi mchezo mzuri na matokeo mazuri kesho,

Vyombo vya habari kutoiongelea Azam FC 

Cioaba alisema tatizo kubwa alilokuwa nalo kuelekea mchezo ni namna vyombo vingi vya habari kushindwa kuiongelea Azam FC na badala yake wamekuwa wakiiongelea sana Simba na kuwaambia kuwa timu yake ni timu kubwa sana tofauti na inavyobezwa.

“Watu wanaiongelea Simba tu kuwa Simba ni timu nzuri na ina kambi nzuri, kila mmoja anaiheshimu Simba pekee, na kuhusu Azam FC imekuwa ikiongelewa kidogo sana, nataka kumkumbusha kila mmoja kuwa Azam FC ni timu inayoshika nafasi ya tatu kwenye ligi na ina pointi 46, imejikusanyia pointi zote uwanjani na sio nje ya uwanja.

“Nimeiongoza Azam FC kwenye mechi 20 hapa, nimepoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Yanga (1-0), lakini hatukuwa na bahati, katika mechi zote hizo sijapata penalti hata moja kwa timu yangu, kwa maoni yangu Azam FC hivi sasa ni timu nzuri sana, inacheza mpira mzuri, na napenda kuiheshimu sana hii timu na wachezaji wake pia, wiki tatu zilizopita timu ya Taifa ilicheza mechi mbili na kushinda zote na wachezaji zaidi ya sita wa Azam FC waliweza kucheza, nashangaa kuona vyombo vya habari vinaiongelea Simba tu hivi sasa,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana, alisema kuwa yeye kama kocha na timu wanaiheshimu Simba kutokana na ukubwa wake hapa nchini na matokeo wanayopata, lakini akaomba kuwa lazima haki na usawa uwe kwa timu zote.

Kauli kwa mashabiki

Mromania huyo alichukua fursa hiyo kuwaomba mashabiki wa Azam FC kujitokeza kwa wingi uwanjani kesho kuishangilia timu hiyo huku akiwakumbusha kuwa watakuwa wakikabiliana na timu ambayo ina mashabiki wengi hivyo ni lazima mashabiki wa timu hiyo nao wajipange kuwasapoti wachezaji wao.

“Mashabiki wote wanaoipenda Azam FC waje kesho kwa pamoja uwanjani, wakae pamoja na kuweka umakini pamoja kwa ajili ya kushinda mchezo huo,” alimalizia.

Ushindi wowote kwa Azam FC kesho utakuwa umeifanya kuingia fainali ya pili mfululizo ya michuano hiyo baada ya mwaka jana kuingia na kupoteza kwa kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Yanga.

Wakati msimu huu ukielekea ukingoni, tayari timu hizo zimekutana mara tatu na Azam FC ikiwa kifua mbele baada ya kushinda mechi mbili na kupoteza moja, mechi hizo mbili ilizoibuka kidedea ya kwanza ilishinda kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi (1-0) kabla ya kupata ushindi kama huo kwenye Ligi Kuu, huku Simba nayo ikishinda ya mzunguko wa kwanza 1-0.

Hivyo wakati timu hizo zikielekea kucheza kwenye mechi yao ya nne msimu huu, kihistoria zimekutana mara 25 katika michuano mbalimbali huko nyuma, Azam FC ikishinda mara tisa, Simba mara 11 huku ikishuhudiwa mechi tano wakienda sare.