NAHODHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, ameweka wazi kuwa wana morali kubwa ya kupata matokeo mazuri kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Sports) dhidi ya Simba Jumamosi ijayo.

Kikosi cha Azam FC kipo kwenye maandalizi makali kuelekea mchezo huo, ambapo tayari kimeshaingia kambini tokea jana katika makao makuu ya klabu hiyo ndani ya viunga vya Azam Complex kujiandaa na mchezo.

Himid ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa kikosi hicho kipo vizuri na watanufaika na urejeo wa wachezaji wao muhimu waliokuwa majeruhi.

“Morali iko juu, timu ipo vizuri bahati nzuri wachezaji wenzetu karibia asilimia 90 wapo vizuri na wapo fiti na wako tayari kwa mchezo na naamini kocha atakuwa na nafasi nzuri ya kuchagua timu yake ya kwenda kucheza mchezo huo,” alisema.

Kiungo huyo anayesifika kwa ukabaji na mwenye mashuti makali, aliongeza kuwa mchezo huo utakuwa mgumu licha ya kufanikiwa kuwafunga mara mbili katika mechi mbili zilizopita.

“Usidhani kama mchezo huu wa tatu utakuwa mrahisi kama mara mbili zilizopita tulizoshinda, kwani Simba nayo inajipanga, lakini naamini sisi tutajipanga vizuri zaidi ili kuweza kushinda mechi hiyo inayokuja,” alisema.

Himid ambaye amekulia kwenye timu hiyo kwa takribani miaka tisa sasa, alitoa wito kwa mashabiki wa Azam FC kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo ili kuwapa sapoti kwani wao ni sehemu muhimu sana katika timu na uwepo wao utawaongezea nguvu zaidi uwanjani ya kuibuka kidedea.