HAYAWI Hayawi sasa yamekuwa! Baada ya ngoja ngoja nyingi, hatimaye sasa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itapambana na Simba katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 29 mwaka huu.

Mbali na mchezo huo wa kwanza wa nusu fainali, pia Mbao itakuwa wenyeji wa Yanga katika mtanange wa pili wa hatua hiyo utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Aprili 30, mwaka huu.

Hafla hiyo ya upangaji droo imefanyika jioni hii katika Ofisi za wadhamini wakuu wa michuano hiyo, Azam Media Limited, zilizopo Tabata, T.O.T, jijini Dar es Salaam, ambapo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa timu hizo nne huku upande wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ukiwakilishwa na mmoja wa maofisa wake, Jemedari Said.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, naye alikuwa kwenye hafla hiyo sambamba na viongozi wengine wa timu hiyo, Meneja wa timu, Phillip Alando na Ofisa Habari, Jaffar Idd.

Nyota wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Idd Moshi ‘Mnyamwezi’, ndio aliyekuwa kinara wa kuendesha droo hiyo iliyopelekea Simba kuwa wenyeji wa Azam FC katika mchezo huo, pamoja na Mbao iliyochaguliwa ya pili kuwa mwenyeji wa Yanga.

Akizungumza kwa ufupi Meneja wa Azam FC, Alando, aliipokea kwa mikono miwili droo hiyo na kuzipongeza timu hizo zilizofika hatua hiyo huku akimshukuru Mungu kwa timu yake kupata nafasi ya kuwa moja ya timu zitakazocheza nusu fainali.

Alando alisema mchezo huo utakuwa mzuri sana huku akitamba kuwa kikosi chao kipo tayari na kitasonga mbele kwa hatua ya fainali.

Hii ni mara ya kwanza kwa Azam FC kukutana na Simba kwenye michuano hiyo, ambapo kwa mwaka huu zimekutana mara mbili na mabingwa hao wa Ngao Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu wamefanikiwa kushinda mechi zote mbili.

Mechi ya kwanza ni ile ya fainali ya Kombe la Mapinduzi ambayo iliifunga bao 1-0 na kutwaa taji hilo, kama ilivyofanya kwenye mchezo wa raundi ya pili ya Ligi Kuu ilipoipa kipigo hicho na kulipa kisasi cha kufungwa mchezo wa raundi ya kwanza kwa ushindi kama huo.