KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, ametuma ujumbe kwa mashabiki wa timu hiyo kuuungana pamoja na timu kuanzia mwezi huu kutokana na umuhimu wa mechi zijazo zinazowakabili.

Azam FC inakabiliwa na mechi tatu muhimu za mwisho za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Kagera Sugar, Toto African na Mbao, ikitakiwa kushinda zote ili kujihakikishia nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Mpaka sasa Azam FC imejikusanyia jumla ya pointi 46 katika nafasi hiyo, ikifukuzana na Kagera Sugar ambayo ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi zake 43 lakini inao mchezo mmoja mkononi.

Mbali na changamoto ya kwenye ligi, mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi mwaka huu wanakabiliwa na mechi ya nusu ta fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) itakayopigwa baadaye mwezi huu na moja ya timu kati ya Mbao, Simba, au mshindi wa robo fainali kati ya Yanga na Tanzania Prisons, itakayofanyika keshokutwa Jumamosi.

Cioaba ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa mechi zote zilizobakia ni muhimu kwa timu yake, hivyo ni wakati mzuri kwa mashabiki wa timu hiyo na watu wote wa Azam FC kuwa pamoja kama familia na kujaa kwa wingi uwanjani ili kuwasapoti wachezaji.

“Timu iko vizuri hivi sasa, napenda mwezi huu kwa pamoja wote tuwe kama familia, napenda kuwaambia mashabiki wote waje kwa wingi kwenye mechi zijazo kuisapoti timu, tuna mwezi mmoja ambao ni mgumu sana kwetu, tuna mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA na pia tuna mechi tatu za nyumbani (za ligi), nahitaji kushinda mechi hizi tatu za ligi ili kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo na pia matarajio yangu makubwa ni kuiongoza Azam FC kuingia kwenye fainali ya Kombe la FA na baadaye kuweka umakini kwa ajili ya kutwaa taji hilo,” alisema.

Azam FC yenye maskani yake kwenye viunga vya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, ipo kwenye mikakati ya kuhakikisha inafanikisha malengo yake hayo ikiwemo kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho (ASFC), ili kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.