KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kucheza mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya African Lyon keshokutwa Jumamosi.

Mchezo huo unaotarajia kuwa mkali na wa aina yake, utafanyika katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 1.00 usiku.

Benchi la ufundi la Azam FC limeandaa mchezo huo, ukiwa ni mahususi kwa ajili ya kukiangalia kikosi chake na kukipima kutokana na kutokuwepo kwa mchezo wowote wa ushindani wikiendi hii.

Azam FC inakabiliwa na mchezo muhimu wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) Aprili 28 mwaka huu, ambapo huenda ikakutana na timu nyingine kati ya Mbao, Simba au mshindi wa mchezo wa robo fainali kati ya Yanga na Tanzania Prisons, itakayofanyika Jumamosi.

Mbali na mechi hiyo, pia kuelekea hitimisho la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu, Azam FC inakabiliwa na mechi tatu za mwisho muhimu dhidi ya Mbao, Kagera Sugar na Toto African, zote zikifanyika kwenye maskani yake ya Azam Complex.

Kwa muda mrefu, Azam FC imekuwa na ikionyeshana ushindani mkali na African Lyon kila zinapokutana, ambapo mchezo huo pia utaendeleza upinzani huo na unatarajiwa kuwa kipimo tosha kwa mabingwa hao Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu.