MAMIA ya Watanzania wamejitokeza jioni ya leo kumzika Baba mzazi wa kiungo nyota wa Azam FC, Frank Domayo, aliyefariki dunia Jumapili iliyopita katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Katika mazishi hayo yaliyofanyika jioni hii katika makaburi yaliyoko Tabata Kifuru, jijini Dar es Salaam, Domayo alipata sapoti kubwa kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo wachezaji, wafanyakazi na viongozi wote kutoka Azam FC.

Viongozi hao wa Azam FC, waliongozwa na Mwenyekiti, Nassor Idrissa ‘Father’, Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Meneja Mkuu Abdul Mohamed na Meneja wa timu, Phillip Alando.

Mbali na uwakilishi huo kutoka Azam FC, pia alikuwemo Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Salum Mayanga, aliyeliwakilisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mara baada ya mazishi hayo, Domayo aliwashukuru watu wote waliohudhuria mazishi hayo na kusema kuwa kama mwanafamilia amepata faraja kubwa kutokana na idadi hiyo kubwa iliyojitokeza kumsapoti.