WAKATI ikiwa imebakiza mechi tatu kuweza kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, juzi ilimaliza mechi yake ya mwisho ugenini kwa kuambulia sare ya mabao 2-2 dhidi ya JKT Ruvu.

Mechi tatu zote za nyumbani ilizobakiza Azam FC ni zile dhidi ya Kagera Sugar, Toto African na Mbao, ambazo zitafanyika kwenye makao makuu yake ya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Kuelekea mechi hizo, mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz unakuchambulia takwimu zote za mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi mwaka huu kwa kuangalia mechi zote 15 walizocheza ugenini na kujua nini walichovuna.

Azam FC katika mechi zake 15 za ugenini imefanikiwa kuvuna jumla ya pointi 23, zikiwa ni nusu ya pointi zote 46 walizovuna hadi sasa kwenye nafasi ya tatu katika msimamo, ambazo zimetokana na ushindi wa mechi sita, sare tano na kupoteza mechi nne.

Kitakwimu wastani wa pointi hizo ilizovuna Azam FC, inaonyesha kuwa wamefanya kazi kubwa ugenini ya kuzoa pointi kwa asilimia 55, huku asilimia zingine 45 zikiwa zimeenda kwenye pointi 22 ambazo wamezipoteza ugenini.

Ukiachana na idadi ya pointi walizovuna, pia katika mechi hizo 15 Azam FC imeweza kufunga jumla ya mabao 17 na kuifanya hadi sasa katika mechi zote walizocheza kuwa na wastani mzuri wa kufunga mabao mengi ugenini tofauti na mechi walizocheza nyumbani.

Aidha katika mabao yote 18 iliyofungwa mpaka sasa kwenye mechi zote, robo tatu ya mabao hayo yote yaani 12 imefungwa katika mechi za ugenini huku ikiwa imeruhusu wavu wake kuguswa mara sita tu nyumbani.

Azam FC katika mechi zote hizo za ugenini, imefanikiwa kuondoka uwanjani bila kuruhusu wavu wake kuguswa katika michezo sita, ikishinda mitatu kati ya hizo na suluhu tatu.

Mfungaji bora wa Azam FC katika mechi za ugenini ni kinda Shaaban Idd, ambaye amefunga jumla ya mabao manne kwenye ligi hiyo msimu huu, yote akifunga ugenini huku akichangia pasi tatu za mwisho zilizozaa mabao mengine, nazo akizitoa ugenini.

Mbali na kufunga idadi hiyo, mpaka sasa kwa mujibu wa takwimu kinda huyo amefunga jumla ya mabao nane msimu huu kwenye mashindano yote, manne kwenye ligi, matatu katika Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na moja akitupia ndani ya michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu.

Kinara wa ufundaji bora wa Azam FC hadi sasa msimu huu, nahodha John Bocco ‘Adebayor’, mwenye mabao 10 kwenye mashindano yote msimu huu, nane Ligi Kuu, moja Kombe la Shirikisho (ASFC) na moja jingine katika Mapinduzi Cup.

Bocco ambaye amekosekana kwenye mechi nyingi za Azam FC mzunguko wa pili, anamfuatia Shaaban kwenye rekodi za mabao ya ugenini katika ligi akiwa amefunga matatu sawa na staa wa zamani wa timu hiyo, Francisco Zekumbawira, lakini nahodha huyo akiwa anaongoza kwa kutoa pasi za mwisho ugenini akiwa ametoa nne.

Mechi zote za Azam FC ugenini (VPL)

Wed 07/09/16 Tanzania Prisons 0 – 1 Azam

Sat  10/09/16  Mbeya City 1 – 2 Azam FC

Sat  24/09/16  Ndanda 2 – 1 Azam FC

Wed  12/10/16 Stand United 1 – 0 Azam FC

Fri  28/10/16  Kagera Sugar 2 – 3 Azam FC

Wed  02/11/16  Toto Africans 0 – 1 Azam FC

Sun  06/11/16  Mbao 2 – 1 Azam FC

Wed  09/11/16  Mwadui 1 – 4 Azam FC

Sun 18/12/16  African Lyon 0 – 0 Azam FC

Sat  24/12/16  Maji Maji 1 – 1 Azam FC

Sat  28/01/17  Simba 0 – 1 Azam FC

Sat  11/02/17  Ruvu Shooting 0 – 0 Azam FC

Sat  01/04/17  Young Africans 1 – 0 Azam FC

Mon  10/04/17  Mtibwa Sugar 0 – 0 Azam FC

Sat  15/04/17   JKT Ruvu  2 – 2 Azam FC

(Win : 6, Draw : 5, Lose : 4)