KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, mchana huu kimeenda kutoa pole kwenye familia ya kiungo wa timu hiyo, Frank Domayo, aliyefiwa na Baba yake mzazi, Raymond Domayo, aliyefaruiki ghafla usiku wa kuamkia leo.

Wachezaji wa Azam FC pamoja na benchi la ufundi na wafanyakazi wengine wa Azam FC, waliokuwemo kwenye msafara wa timu hiyo uliotokea jijini Tanga kucheza dhidi ya JKT Ruvu jana, walimsindikiza Domayo na kujumuika naye katika kuomboleza kifo hicho.

Kutokana na Azam FC kuguswa kwa moja kwa moja kwenye msiba huo, uongozi utaendelea kuwa pamoja na Domayo kwa hali na mali, na ndugu, jamaa na marafiki wanohusika na msiba huo katika kipindi hiki kigumu.

Kwa mujibu wa Wanafamilia, mazishi ya Mzee Domayo yatafanyika keshokutwa Jumanne maeneo ya Kifuru, Tabata, ambapo familia ya Azam FC itajumuika naye katika kuupumzisha mwili huo katika nyumba ya milele.

Katika kufanikisha shughuli zote za mazishi, uongozi wa Azam FC umetoa basi lake dogo kwa ajili ya kusafairisha watu watakaokwenda kwenye mazishi hayo huku ikiangalia namna nyingine ya kiutawala katika kusaidia sehemu nyingine ya kufanikisha zoezi hilo.

Azam FC inawaomba mashabiki wote wa timu hiyo na wadau wa soka nchini kumuunga mkono nyota huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa kujumuika naye kwa siku ya keshokutwa katika mazishi hayo.