LICHA ya kukumbana na maamuzi mabovu ya waamuzi kwenye mchezo wa leo, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanikiwa kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya JKT Ruvu, mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Sare hiyo inaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 46 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa imezidiwa pointi 16 na kinara Simba alikuwa nazo 62, huku JKT ikibakia mkiani kwa kujiongezea alama moja na kufikia 22.

Mchezo huo kwa kiasi kikubwa uliathiriwa na mvua ambayo ilinyesha muda mwingi wa mchezo huo na kufanya uwanja kuwa na utelezi wa matope kiasi kwenye baadhi ya maeneo.

Azam FC ndio iliyoanza kulitia kashikashi lango la wapinzani wao kwa kutengeneza nafasi nzuri dakika ya nne na saba kupitia kwa Gadiel Michael na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ lakini kipa alikuwa vema kuondoa hatari zote hizo.

Dakika 13 kama mshambuliaji kinda wa timu hiyo, Shaaban Idd, angekuwa makini angeweza kuipa bao la uongozi Azam FC lakini shuti alilopiga akiwa ndani ya eneo la 18 lilipaa juu ya lango.

Shaaban alirekebisha makosa yake dakika mbili baadaye kwa kuipatia bao la uongozi Azam FC kwa shuti la kiufundi akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na winga Ramadhan Singano ‘Messi’, aliyewatoka mabeki kadhaa kwa kasi kabla ya kutoa pande hilo.

Mshambuliaji huyo aliyesimamisha peke yake mbele kutokana na mastraika wengine kuwa majeruhi, alikosa nafasi ya wazi dakika ya 17 baada ya kuingia vema ndani ya eneo la 18 lakini shuti alilopiga lilipaa juu ya lango.

JKT Ruvu walifanikiwa kusawazisha kupitia kwa Mussa Juma, dakika ya 25 kabla ya Frank Nchimbi kuongeza la pili kwa kichwa dakika sita baaadaye na hivyo kuifanya JKT Ruvu kuondoka kifua mbele kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kuendeleza kasi ya kusaka bao la kusawazisha na dakika ya 57 ilifanya mabadiliko ya wachezaji wawili kwa mpigo wakiingia Abdallah Masoud na Joseph Mahundi na kupumzishwa Gadiel Michael na Ramadhan Singano.

Mabadiliko hayo yaliiongeze uhai Azam FC kwenye eneo la kiungo kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha kinda Masoud, hali iliyowafanya JKT Ruvu kupoteza muda mara kwa mara kwa wachezaji wake kujiangusha na kuchelewa kuicheza mipira ya kurusha na faulo.

Huku pia waamuzi wakiwa kigingi kingine kwa Azam FC kutokana na kuchezesha hovyo kwa kushindwa kutafsiri sharia 17 za soka kwa makusudi hasa katika eneo la mipira ya kuotea, wakionekana wamedhamiria mchezo huo umalizike kwa mabingwa hao kupoteza.

Alikuwa ni beki Erasto Nyoni, aliyetumia jitihada binafsi kuisawazishia Azam FC dakika ya 75 kwa bao safi la shuti la umbali wa mita takribani 25 lililomshinda kipa na kutinga wavuni.

Azam FC ingeweza kujipatia mabao zaidi kama kiungo Frank Domayo, angeweza kuitumia vema nafasi aliyopata dakika za mwisho baada ya kuwazidi maarifa mabeki wa JKT Ruvu na kupata uwazi wa kuonana na kipa lakini shuti alilopiga lilipaa juu ya lango.

Huo ulikuwa ni mchezo wa mwisho kwa Azam FC ugenini msimu huu, ambapo mechi zote tatu zilizobakia kukamilisha msimu itacheza nyumbani Azam Complex dhidi ya Kagera Sugar, Toto African na Mbao.

Kikosi hicho kitaanza rasmi safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho asubuhi tayari kabisa kujiandaa na mechi zijazo.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa hivi:

Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael/Joseph Mahundi dk 57, Daniel Amoah, David Mwantika, Himid Mao (C), Ramadhan Singano/Masoud Abdallah dk 57, Frank Domayo, Shaaban Idd/Mudathir Yahya dk 85, Salum Abubakar, Bruce Kangwa