KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo Jumamosi saa 10.00 jioni inatarajia kumaliza mchezo wake wa mwisho ugenini kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kuvaana na JKT Ruvu katika Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Tayari kikosi cha Azam FC chenye morali kubwa kipo kamili kwa mchezo huo na jioni ya jana kilifanya mazoezi ya mwisho ndani ya uwanja huo utakaochezewa mechi hiyo, huku Kocha Mkuu, Aristica Cioaba, akisema wapo tayari kwa mapambano ya kuwania poiti zote tatu.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi hayo, Cioaba alisema ijapokuwa anawakosa nyota wake watano wazoefu kwenye kikosi hicho, lakini amejipanga kusaka matokeo mazuri kupitia wachezaji vijana aliowaandaa.

“Bado naendelea kusisitiza kuwa nitawapa nafasi wachezaji vijana katika mchezo huo kwa manufaa ya klabu hapo baadaye, nawaamini wachezaji vijana watatimiza lengo kwa kupata matokeo mazuri kesho,” alisema.

Wachezaji watakokosekana kwenye mchezo huo ni mabeki Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, kiungo Stephan Kingue na washambualiaji, Yahaya Mohammed na John Bocco ‘Adebayor’, ambaye ni nahodha wa kikosi hicho, ambapo wote bado wanaendelea na programu maalum kabla ya kurejea dimbani.

Katika mchezo huo, Azam FC inatarajia kuimarika kwenye eneo lake la kiungo kwa kunufaika na urejeo wa kiungo wake Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye alikosekana katika mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar kutokana na kukusanya kadi tatu za njano.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi mwaka huu, wanaoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wakiwa na pointi 45 wataingia dimbani kuwania pointi tatu ili kuendelea kufukuzia nafasi tatu za juu, huku wapinzani wao JKT Ruvu walikuwa mkiani kwa pointi 22 nao wakipigania ushindi ili kujinasua katika janga la kushuka daraja.