KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki Kati, Azam FC, imetoka sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ukiofanyika Uwanja wa Manungu, Turiani, mkoani Morogoro.

Sare hiyo imeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 45 na kubakia katika nafasi ya nne kwenye msimamo, ikiwa nyuma ya pointi 13 na Simba iliyofikisha 58, Yanga ambayo ina mchezo mmoja mkononi ni ya pili ikiwa nazo 56 huku Kagera Sugar ikikamata ya tatu kwa pointi zake 46.

Hiyo ni sare ya tatu baina ya timu hizo kwenye mechi tisa walizokutana ndani ya uwanja huo, katika mechi zilizobakia Azam FC imeshinda mara tano na kufungwa mmoja, huku katika rekodi ya mechi 18 za ligi walizokutana, mabingwa hao wakiwa wameshinda mara tisa, Mtibwa mara mbili na mechi sita wakienda sare.

Azam FC iliingia kwenye mchezo huo ikiwakosa nyota wake sita wa kikosi cha kwanza, mabeki Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, kiungo Stephan Kingue, nahodha John Bocco na Yahaya Mohammed, wote wakiwa majeruhi huku kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ akiwa anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

Ili kuendana na wachezaji walioko kikosini, Koch Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alilazimika kubadilisha mfumo kutoka 4-3-3 aliokuwa akitumia kwenye mbalimbali zilizopita hadi 3-4-3, uliomlazimu kutumia mabeki watatu wa kati ambao ni Erasto Nyoni, Daniel Amoah na David Mwantika huku katika ushambuliaji akimtegemea pekee kinda Shaaban Idd.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi, walifanikiwa kucheza vema kipindi cha kwanza na kufanikiwa kutengeneza nafasi nne hadi tano ambazo zingeweza kuwapatia mabao, lakini zilishindwa kutumiwa vema.

Mfano katika dakika ya saba, Shaaban alikuwa kwenye nafasi nzuri ya kumtengenezea bao Joseph Mahundi akiwa ndani ya eneo la hatari, lakini pasi aliyopiga ilipita nyuma ya winga huyo kabla ya mabeki wa Mtibwa Sugar kuokoa shambulizi hilo la hatari langoni mwao.

Nafasi nyingine muhimu ni ile ya dakika ya 32, ambapo Mahundi aliambaa na mpira na kuwatoka wachezaji wa Mtibwa kabla ya kuhamisha mpira huo kwa Ramadhan Singano ‘Messi’, lakini shuti alilopiga Frank Domayo, lilipaa juu ya lango.

Dakika ya 42, Mahundi alipiga shuti zuri akiwa nje kidogo ya eneo la 18, ambalo lilitoka sentimita chache ya lango, winga huyo alipata nafasi hiyo baada ya kupigiwa krosi safi na Singano na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika bado milango ya pande zote mbili ilizidi kuwa migumu.

Kipindi cha pili, Azam FC ilifanya mabadiliko ya wachezaji wawili kwa nyakati tofauti, safu ya ushambuliaji ikiimarishwa kwa kutoka Samuel Afful na kutoka Mahundi, mabadiliko ambayo yalishindwa kufanya kazi kama ilivyotarajiwa na benchi la ufundi na baadaye dakika za mwisho aliingia Abdallah Kheri na kutoka Singano, ili kuimarisha eneo la ulinzi.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC, keshokutwa Jumatano kinatarajia kuanza rasmi mazoezi ya maandalizi ya mchezo ujao wa ligi dhidi ya JKT Ruvu, unaotarajia kufanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumapili ijayo saa 10.00 jioni.

Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Daniel Amoah, David Mwantika, Himid Mao (C), Joseph Mahundi/Afful dk 59, Frank Domayo, Shaaban Idd, Ramadhan Singano/Abdallah dk 88