KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho Jumatatu saa 10.30 jioni itakuwa na shughuli pevu pale itakapokuwa ikivaana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.

Azam FC tayari imeshawasili mkoani Morogoro tayari kabisa kwa mchezo huo na leo jioni itakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri kufanya mazoezi yake ya mwisho kuelekea mtanange huo unaotarajia kuwa mkali na wa aina yake.

Wakati Azam FC ikiingia uwanjani na morali kubwa baada ya kutoka kuichapa Ndanda mabao 3-1 kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na kutinga hatua ya nusu fainali, Mtibwa Sugar imetoka kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa ligi uliofanyika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Azam FC itaendelea kukosa huduma za wachezaji wake wanne ambao ni majeruhi, mabeki Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, kiungo Stephan Kingue na mashambuliaji Yahaya Mohammed, huku kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, akikosekana kutokana na kukusanya kadi tatu za njano.

Rekodi zao muhimu

Kuelekea mchezo huo, hizi hapa ndio takwimu za timu hizo kwenye mechi za mashindano mbalimbali zilizokutana, ambazo zinaonyesha kuwa wamekutana mara 20, zikiwa ni mechi 17 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), moja ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na mbili za Kombe la Mapinduzi.

Katika mechi 17 za ligi walizokutana tokea Azam FC ipande daraja mwaka 2008, matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex ndio wanarekodi bora wakiwa wameshinda robo tatu ya mechi hizo yaani mara tisa, Mtibwa Sugar ikishinda mara mbili tu na michezo sita wakienda sare.

Kati ya mechi hizo, nane wamecheza ugenini kwenye Uwanja wa Manungu, Azam FC imeonekana kuwa rekodi bora zaidi kuliko zile za nyumbani kwa kupata matokeo bora zaidi, ambapo imefanikiwa kushinda mechi tano, ikafungwa mmoja na kuambulia sare mbili.

Ushindi unaokumbukwa zaidi kuwahi kuupata Azam FC dhidi ya Mtibwa Sugar ni ule walioibugiza mabao 5-2 msimu wa 2014/15, pia wakiwa na rekodi ya kuwatungua wakatamiwa hao 4-0 msimu wa 2010/2011.

Katika mechi hizo 17 za ligi, jumla ya mabao 38 yamefungwa ukiwa ni wastani wa kufungwa mabao 2.2 katika kila mchezo, Azam FC ikiwa inaongoza ikiwa imetupia 26 huku Mtibwa Sugar ikiuona wavu wa matajiri hao mara 12 tu.

Mwezi uliopita, Azam FC ilikipiga dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa hatua ya 16 ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu, wakichomoza na ushindi wa bao 1-0, lililowekwa kimiani na Ramadhan Singano ‘Messi’, ambaye yupo kwenye kiwango cha juu hivi sasa akiwa amefunga mabao matatu katika mechi nne zilizopita za mashindano mbalimbali.

Mara mbili walizokutana kwenye Kombe la Mapinduzi, mwaka juzi zilitoka sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 kwenye robo fainali na Azam FC kutolewa kwa mikwaju ya penalti 7-6 huku mwaka jana zikitoka sare kama hiyo katika mchezo wa hatua ya makundi.

Msimu huu katika mzunguko wa kwanza wa ligi zilikutana ndani ya Azam Complex na kutoka sare ya bao 1-1, bao la Azam FC likifungwa kwa mkwaju wa penalti na Nahodha Msaidizi, Himid Mao ‘Ninja’ huku Mtibwa iliyotangulia kupata bao ikijipatia kupitia kwa mshambuliaji, Rashid Mandawa, aliyewahi kuchezea timu ya vijana ya Azam FC.

Mbali na kuwa na Mandawa, pia Mtibwa Sugar inao kiungo Ibrahim Jeba, aliyewahi kulelewa kwenye kituo cha Azam Academy huku pia wakiwa na mshambuliaji wa Azam FC, Kelvin Friday, ambaye yuko kwa mkopo wa msimu mzima akitokea kwa matajiri hao.