KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, jioni ya leo kimeanza rasmi kazi ya kusaka pointi tatu dhidi ya Mtibwa Sugar baada ya kuanza mazoezi ya kujiweka sawa kuelekea mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro Jumatatu ijayo.

Azam FC inaanza maandalizi hayo ikiwa na morali kubwa baada ya juzi kuichabanga Ndanda mabao 3-1 na kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Timu hiyo imeanza mazoezi ikiwa bila ya wachezaji wake wawili, mshambuliaji Yahaya Mohammed, ambaye ni majeruhi na Yakubu Mohammed, aliyeumia kwenye mchezo dhidi ya Ndanda, huku nyota wengine watatu nahodha John Bocco ‘Adebayor’, beki Aggrey Morris na kiungo Stephan Kingue, wakiendelea na mazoezi mepesi ya kujiweka sawa kabla ya kuruhusiwa kurejea uwanjani.

Kikosi hicho kinatarajia kuendelea tena na mazoezi kesho Jumamosi asubuhi kabla ya mchana kuanza safari ya kuelekea mkoani Morogoro kwa mchezo huo, kikiwa na lengo la kuzoa pointi zote tatu ili kuwania nafasi za juu ya msimamo wa ligi hiyo.

Itakumbukwa ya kuwa kwenye mchezo wa raundi ya kwanza timu hizo zilitoshana nguvu kwa sare ya bao 1-1, bao la Azam FC likiwekwa wavuni ya nahodha John Bocco ‘Adebayor’ huku Mtibwa ikitangulia kufunga kupitia kwa nyota wa zamani wa timu ya Academy ya Azam FC, Rashid Mandawa.

Hata hivyo zilipokutana mwaka huu kwenye hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la FA, Azam FC iliibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0, lililowekwa kimiani na winga machachari anayerejea kwa kasi, Ramadhan Singano ‘Messi’.