KUFANYA vizuri kwa wachezaji vijana katika mchezo wa jana wa Azam FC dhidi ya Ndanda, kumemfurahisha Kocha Mkuu wa Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, Aristica Cioaba, ambaye hakusita kusema amepanga kuwapa nafasi zaidi hapo baadaye ndani ya timu hiyo.

Mshambuliaji kinda wa timu hiyo, Shaaban Idd, aliwaongoza vibana wenzake kufanya kweli jana baada ya kuiongoza Azam FC kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) kufuatia kuitungua Ndanda mabao 3-1, yeye akifunga mawili na Ramadhan Singano ‘Messi’, akitupia la mwisho.

Kocha Cioaba, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz namna alivyomuandaa Shaaban hadi kuibuka mfungaji wa mabao hayo muhimu ya timu hiyo usiku wa jana akisema alimpa maelekezo mazuri ya kufanya akiwa karibu ya lango ambayo ameyatumia vema.

“Niliwaingiza wachezaji vijana ndani ya uwanja, mimi nawapenda wachezaji vijana niliweza kuongea na Shaaban (Idd) baada ya kupata nafasi mbili kwenye mchezo uliopita dhidi Yanga na kushindwa kuzitumia, hivyo nilimwambia ukiingia uwanjani leo na ukaweza kujiamini mwenyewe utafunga mabao na ameweza kufanya kweli na kufunga mabao mawili mazuri leo.

“Mimi ni aina ya kocha ninayependa kuwapa fursa wachezaji vijana na hapo baadaye natarajia kuwapa nafasi zaidi katika timu hii, mimi ni aina ya kocha ninaowapenda mashabiki nawaomba wazidi kuja uwanjani kwani ukiiangalia hii timu inawachezaji wengi vijana wanaoihitaji sapoti yao, napenda kuwaahidi nitajaribu kadiri ya uwezo wangu ili hapo baadaye timu hii iwe na matokeo mazuri,” alisema.

Cioaba aliwapongeza wachezaji wake kwa kufanikisha ushindi huo, huku akielezea hali mbaya kwenye kikosi chake baada ya wachezaji takribani sita kuingia kwenye orodha ya wachezaji majeruhi.

“Hao ni wachezaji sita muhimu wa Azam FC, lakini wachezaji wengine vijana waliingia uwanjani kama vile Shaaban kama ulivyoona nimempa nafasi na nimefurahishwa baada ya kufunga na bao jingine limefungwa na Messi (Ramadhan Singano) ambaye ni mchezaji mzawa, kama wakiendelea kutilia mkazo na kuendelea na hali hii, timu hii hatua kwa hatua itacheza mchezo mzuri na kuwa na matokeo mazuri na hii inahitaji muda,” alisema.

Alisema anachosubiria hivi sasa ni kurejea kwa wachezaji wake waliokuwa majaruhi, ambapo amedai kuwa Bocco, Stephan Kingua na Aggrey Morris, wote kwa pamoja wanaweza kurejea baada ya wiki moja hali ambayo itazidi kuimarisha kikosi chake kuelekea mechi zijazo.

“Kama nitakuwa na kikosi kamili, nafikiri kasi ya kikosi changu itabadilika, nina muda wa kujiandaa kuelekea mchezo ujao wa nusu fainali, lakini sasa hivi unakuja mchezo wa ligi baada ya siku nne zijazo na akili yangu yote ipo kwenye mchezo huo,” alisema.

Kocha huyo raia wa Romania, aliyetoka kuifunza Aduana Stars ya Ghana msimu uliopita, alimalizia kwa kusema kuwa anapenda kuiona timu yake ikisonga mbele na kuingia fainali na kisha kutwaa taji hilo huku akikiri kuwa mtihani huo hautakuwa rahisi kama watu wanavyofikiria kutokana na kuwa na uwezekano wa kucheza na timu kubwa hapa Tanzania.