BAADA ya kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Federation Cup), winga machachari wa kushoto wa Azam FC, Ramadhan Singano ‘Messi’, ameweka wazi kuwa hawaangalii anayekuja mbele yao bali wamejipanga kufanya vizuri katika kila mchezo.

Azam FC kwa kutinga hatua hiyo kwa kuichapa Ndanda mabao 3-1 usiku wa kuamkia leo, imekata tiketi ya kukutana na Mbao, Simba ambao tayari wameingia hatua hiyo au mshindi wa mchezo wa robo fainali ya mwisho kati ya Yanga na Tanzania Prisons, utakofanyika Aprili 22 mwaka huu.

Mabao ya Azam FC yalifungwa kiufundi na mshambuliaji Shaaban Idd, aliyetupia mawili na Singano akitupia la mwisho lililomfanya kutimiza mabao matatu ndani ya mechi nne zilizopita za mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati za mashindano yote.

Singano ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa siri kubwa ya ushindi huo ni kujituma kwa wachezaji wote na umoja uliopo ndani ya timu hiyo kuanzia viongozi, mashabiki hadi wachezaji.

“Tunamshukuru Mungu kwa kupata matokeo mazuri, siri ya matokeo ya leo naamini ni kujituma kwa wachezaji wote na umoja uliopo ndani ya timu kuanzia viongozi, mashabiki hadi wachezaji na siri ya bao langu ni ushirikiano uliopo baina ya wachezaji wote katika mchezo wa leo,” alisema nyota huyo aliyepachikwa jina la staa wa Barcelona na Argentina, Messi, kutokana na kasi yake uwanjani na uwezo wa kuchachafya wachezaji wa timu pinzani.

Singano alisema hawataangalia anayekuja mbele yao katika hatua ijayo bali wanachoangalia ni kuendelea kufuata maelekezo ya kocha wao, Aristica Cioaba, na kuzingatia kile ambacho anakihitaji kocha ili kuendelea kufanya vizuri katika kila mchezo wanaocheza.

Tokea alipoanza kuaminiwa na Cioaba kwa kuwekwa kikosi cha kwanza, Singano amefanikiwa kutumia vema nafasi hiyo kwa kuonyesha kiwango kizuri kila kukicha jambo ambalo limekuwa likimfurahisha kocha huyona kumpa namba ya kudumu upande wa kushoto kwenye kila mechi ya timu hiyo.