MSHAMBULIAJI kinda wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shaaban Idd, amesema kuwa kupangwa kwenye nafasi ya ushambuliaji katikati kumemfungulia zaidi njia ya kufunga mabao tofauti na mechi kadhaa zilizopita kuchezeshwa akitokea pembeni.

Kauli hiyo ya Shaaban inakuja baada ya kuiongoza Azam FC kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mwadui huku yeye akitupia nyavuni mawili na jingine likifungwa na Ramadhan Singano ‘Messi’.

“Kwanza namshukuru Mungu kwa kufanikiwa kuipa ushindi timu yangu, pili mchezo haukuwa mrahisi, ulikuwa mgumu kama tulivyokuwa tunaona lakini tunashukuru Mungu wachezaji wote tumefuata maelekezo ya mwalimu, tumepambana, hatimaye tumeweza kuibuka na ushindi,” alisema Shaaban wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz

Licha ya kutofunga mabao katika mechi kadhaa zilizopita alizokuwa akiingia kipindi cha pili na zingine baadhi kuanza, Shaaban alisema kuwa yeye ni yule yule wa kawaida isipokuwa utofauti na namba anayochezeshwa, wakati mwingine akicheza pembeni sana lakini jana akianzia katikati na kufunga mabao.

Shaaban alipata nafasi hiyo ya kuwekwa katikati baada ya kuumia kwa mshambuliaji aliyekuwa akitegemewa wa timu hiyo, Yahaya Mohammed, kwenye mchezo uliopita dhidi ya Yanga, ambaye ameongeza wimbi la majeruhi kwenye nafasi hiyo kufuatia nahodha John Bocco ‘Adebayor’, naye kusumbuliwa na nyama za paja kwa takribani wiki tatu na nusu sasa.

Mshambuliaji huyo alichukua fursa hiyo kutoa zawadi ya mabao yake kwa timu hiyo, familia yake pamoja na mashabiki wa mabingwa hao huku akiomba sapoti yao kubwa ya kumuunga mkono, na kuelezea staili yake ya kushangilia mabao akisema kuwa: “Ujue mchezaji wa mpira ukiacha kazi ya uwanjani, lazima uwe na kitu chako mwenyewe ndio ingawa wanafanya wachezaji wengi kushangilia hivyo, lakini nimeamua tu siku ya leo nikifunga goli nishangilia hivi.”

Kinda huyo aliyekulia kwenye kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC, alizungumzia hatua ya nusu fainali waliyoingia na kusema kuwa: “Sisi yoyote anakuja mbele yetu tumejipanga vizuri kwa sababu programu zetu ziko vizuri, mwalimu wetu anatuandaa vizuri kwa hiyo hatuna shaka na mtu yoyote anayekuja mbele yetu.”

Mabao mawili aliyofunga Chilunda, yamemfanya kufikisha mabao matatu kwenye michuano hiyo na sita msimu huu kwenye mashindano yote, matatu akiwa amefunga Ligi Kuu na moja jingine akitupia wakati Azam FC ikiilaza Cosmo Politan 3-1 katika FA Cup.