KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, usiku huu imetinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) kwa kishindo baada ya kuipiga Ndanda mabao 3-1, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Shujaa wa Azam FC katika mchezo huo alikuwa ni mshambuliaji kinda Shaaban Idd, aliyefunga mabao mawili huku jingine likisukimizwa wavuni na Ramadhan Singano ‘Messi’.

Azam FC iliuanza mchezo huo kwa kasi ikicheza soka la kasi na kufanya mashambulizi matatu ya hatari na kufanikiwa kupata bao la uongozi dakika ya 13, lililofungwa na Shaaban aliyemzidi maarifa kipa wa Ndanda, Jeremiah Kisubi.

Dakika moja baadaye Ndanda alisawazisha bao hilo kupitia kwa William Lucian, aliyepiga shuti la moja kwa moja baada ya kipa wa Azam FC, Aishi Manula, kuokoa mchomo mkali wa nguvu kwa ngumi uliokuwa umeelekezwa langoni mwake.

Dakika ya 17 Azam FC ilipata pigo na kulazimika kufanya mabadiliko baada ya kuumia kwa beki wake, Yakubu Mohammed, ambapo nafasi yake ilichukuliwa na David Mwantika dakika ya 20.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu, walizidi kuendeleza kasi yao kwenye lango la Ndanda, dakika ya 22 ilifanya shambulizi kali baada ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’, kupiga pasi safi ya juu iliyookolewa vibaya na kipa, lakini shuti alilopiga Frank Domayo, liliokolewa na mabeki.

Alikuwa ni Shaaban tena aliyeendeleza kilio kwenye lango la Ndanda, baada ya kufunga Azam FC bao safi dakika ya 44 kufuatia kuwazidi ujanja mabeki na kuunyanyua mpira uliompita kipa na kujaa wavuni na kufanya Azam FC iende mapumziko ikiwa kifua mbele kwa mabao hayo.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na ndani ya dakika ya kwanza ya kipindi hicho, Singano aliyekuwa kwenye kiwango bora hivi sasa aliihakikishia ushindi Azam FC kwa kufunga bao zuri baada ya kupiga krosi iliyojaa moja kwa moja wavuni.

Hilo ni bao la tatu la Singano ndani ya mechi nne zilizopita za michuano yote, mengine akifunga kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora ya michuano hiyo Azam FC ilipoifunga Mtibwa Sugar 1-0, huku pia akitupia walipopata ushindi kama huo dhidi ya Mbabane Swallows.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kuwa kwenye nafasi ya kukutana na timu nyingine kama vile Mbao, Simba ambazo nazo zimetinga hatua hiyo au mshindi wa mchezo mwingine wa robo fainali kati ya Yanga na Tanzania Prisons utakaofanyika Aprili 22.

Mara baada ya mchezo huo kikosi cha Azam FC kitakuwa na mapumziko kesho Alhamisi kabla ya kurejea tena mazoezini keshokutwa Ijumaa kuanza maandalizi ya kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika Uwanja wa Manungu, Morogoro Jumatatu ijayo.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa hivi:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Yakubu Mohammed/David Mwantika dk 20, Daniel Amoah, Himid Mao (C), Salum Abubakar, Frank Domayo, Samuel Afful/Khamis Mcha dk 64, Shaaban Idd, Ramadhan Singano/Bruce Kangwa dk 89