KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo asubuhi ilifanya ziara kwa wadhamini wake wakuu Benki ya NMB, ambayo imeonyesha kuridhishwa na udhamini wake kwa mabingwa hao.

Azam FC imetumia ziara hiyo kujifunza mambo mbalimbali yaihusuyo benki hiyo inayoongoza nchini kwa sasa, ikiwemo kuwapelekea makombe matatu waliyopata kipindi cha udhamini wa NMB kuanzia msimu wa 2014-2015 ilipoanza hadi sasa.

Baadhi ya vikombe hivyo ni taji la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) iliyolitwaa mwaka juzi, Ngao ya Jamii waliyoibeba mwaka jana, Kombe la Mapinduzi mwaka huu na lile taji la michuano ya Vijana ya Afrika Mashariki mwaka jana.

Msafara wa Azam FC ulioongozwa na Meneja wa timu, Phillip Alando, ulikuwa na timu kubwa na ile ya vijana ya chini ya umri wa miaka 20 (U-20) na makocha wote pamoja na viongozi wakuu, Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba na Meneja Mkuu, Abdul Mohamed.

Ikiwa ndani ya viunga vya makao makuu wa NMB, Posta, Dar es Salaam, kikosi hicho kilipata fursa ya kutembezwa kwenye maeneo mbalimbali ya benki hiyo, ziara ambayo wachezaji na benchi la ufundi waliweza kujifunza vitu mbalimbali pamoja na kupiga picha za ukumbusho na wenyeji wao.

Akitoa neno lake wakati akiikaribisha timu hiyo, Afisa Mkuu wa Fedha NMB, Waziri Barnabas, alisema kuwa wanayofuraha kubwa kuendelea na udhamini wao huo huku akiipongeza Azam FC kwa mafanikio wanayoendelea kupata na kuwaomba waendelee kuongeza juhudi.

“Leo sisi ni furaha kuwaona wachezaji wakiwa hapa, tunawapa hongera sana kwa mafanikio mnayoendelea kupata, na muendeleze juhudi tunatarajia makubwa kutoka kwa Azam na tunaona itakuja kuwa ni timu ambayo ni ya mfano Tanzania na Afrika kwa ujumla, kwa hiyo hongera mnayo sapoti yetu kwa ujumla, tunafuraha sana leo mmeweza kutuletea baadhi ya makombe ambayo mmepata na wafanyakazi wetu wamefurahi kuwa pamoja na nyie,” alisema.

Barnabas alisema kuwa waliamua kufanya kazi na Azam FC kwa sababu ya kuwa wanaamini ni timu imara, huku akiusifia uongozi wa timu hiyo, akisema kuwa: “Iko chini ya uongozi imara bwana Saad (Kawemba) na benchi lote pamoja na uongozi wote wa Azam FC.”

Azam FC nayo yanena

Akiongea kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC, Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, aliushukuru uongozi wa NMB kwa kuendelea na udhamini huo huku akidai kuwa kupitia ushirikiano wao wamefanikiwa kutimiza mambo mengi ya maendeleo ya timu hiyo.

“Huu udhamini tunaouzungumza ni ushirikiano ambao umetusogeza sana Azam FC na tunaamini kabisa kwamba baada ya muda mfupi watu wengine kukimbia kuona kwamba inakuaje kwanini Azam FC na sio wengine? Lakini siri ni moja tu kutengeneza mfumo wako mzuri, kila kitu kiwe na uwazi, uwajibikaji uwe unaonekana, halafu baada ya hapo watu watakuja kufanya kazi na wewe,” alisema.

Kawemba alizungumzia mafanikio waliyopata katika kipindi chote hiki cha udhamini huo na kudai kuwa kwa misimu yote mitatu hawajakwenda si chini ya nusu ya malengo waliyojiwekea.

“Ushirikiano wetu unakwenda msimu wa tatu huu, katika muda huo Azam FC tumepata mafanikio vizuri sana, na kila malengo tukiweka hatuendi sio chini ya nusu ya malengo hayo, usipojisifia hakuna atakayekusifia kama Tanzania inasimama leo, klabu pekee ambayo ina makombe msimu huu kwa Tanzania ni Azam FC.

“Hakuna klabu yoyote nyingine Tanzania yenye makombe msimu huu, hivyo ni mafanikio ambayo kama klabu na wadhamini wetu (NMB), tunayofahari ya kujivunia kwa sababu sisi ndio tumechukua Ngao ya Jamii kwenye kufungua msimu tunayosisi, sisi ndio tumechukua Kombe la Mapinduzi na bado kwenye Kombe la FA tupo kwenye robo fainali na kitu chochote kinaweza kutokea na bado tupo katika ligi,” alisema.

Kwa mara ya kwanza NMB kuipa udhamini Azam FC, ilikuwa ni mwanzo mwa msimu wa 2014/15 ukiwa ni wa miaka miwili baada ya kutwaa taji la kwanza la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) 2013/14 kwa rekodi ya kutopoteza mchezo wowote, udhamini ambao umeongezwa tena msimu huu.