LICHA ya kucheza soka zuri kwa vipindi vyote na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao, Azam FC imejikuta ikiteleza na kufungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kubakiwa na pointi zake 44, Yanga ikipanda hadi kileleni mwa msimamo baada ya kufikisha pointi 56 ikiizidi Simba pointi moja (55), ambayo imeangukia nafasi ya pili.

Azam FC itabidi ijilaumu katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo baada ya washambuliaji wake, Yahaya Mohammed na Shaaban Idd, kujikuta wakishindwa kuzitumia vema nafasi takribani nne zilizotengenezwa.

Moja ya kosakosa hizo ni dakika ya 26, ambapo Yahaya alipata nafasi nzuri kufuatia pasi ya Ramadhan Singano ‘Messi’, lakini akachelewa kupiga na mabeki wa Yanga kuokoa miguuni mwake.

Kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye anastahili kuwa mchezaji bora wa mchezo huo, naye alishindwa kuipa bao la uongozi timu hiyo akiwa ndani ya eneo la hatari baada ya kupiga shuti lililotoka pembeni kidogo ya lango, kashikashi iliyotokana na mpira mzuri wa krosi uliopigwa na Gadiel Michael, kuokolewa vibaya na mabeki.

Kiukweli katika mchezo huo, Azam FC ilifanikiwa kuutawala kufuatia viungo Salum, nahodha msaidizi Himid Mao na Frank Domayo, kuwazidi maarifa viungo wa Yanga waliokuwa wakiongozwa na Haruna Niyomzima.

Azam FC ililazimika kufanya mabadiliko dakika ya 43 ya mchezo baada ya kuumia mguu kwa Yahaya wakati akipiga shuti, na nafasi yake ilichukuliwa na mshambuliaji mwingine Samuel Afful.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu zote zilitoka uwanjani zikiwa sare, ambapo kipindi cha pili Azam FC ilianza na kasi yake ile ile iliyoanza nayo kipindi cha kwanza, na kama Singano angekuwa makini huenda angeipa bao la uongozi dakika ya 46, lakini alichelewa kupiga mpira na mabeki kuokoa.

Singano alipata nafasi hiyo nzuri, iliyotokana na shuti alilopiga Shaaban kupanguliwa vibaya na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi, na mpira kutua kwenye eneo alilokuwa winga huyo.

Uzembe wa eneo la ulinzi la Azam FC kushindwa kuokoa mpira uliopigwa na Niyonzima katika dakika ya 70, uliweza kuizawadia Yanga bao, lililofungwa na mshambuliaji wao, Obrey Chirwa.

Bao hilo la Chirwa limehitimisha rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Azam FC ya kutopoteza mchezo wowote kwenye ligi mwaka huu, huku ikicheza mechi saba mfululizo bila kuruhusu wavu kuguswa.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaendelea na mazoezi kesho Jumapili jioni kujiandaa na mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Ndanda, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku

Kikosi cha Azam FC leo

Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Daniel Amoah, Yakubu Mohammed, Himid Mao, Salum Abubakar, Frank Domayo, Yahya Mohmmed/Samuel Afful dk 44, Shaaban Idd/Bruce Kangwa dk 75 na Ramadhan Singano/Joseph Mahundi dk 69