MSHAMBULIAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Yahaya Mohammed, jana amefanya kitu kikubwa kwenye jamii ya Tanzania, baada ya kutoa msaada kwenye kituo cha watato yatima cha ‘Hisani Orphanage’ kilichopo Mbagala Maji Matitu, jijini Dar es Salaam.

Nyota huyo kutoka Ghana aliyeongozana sambamba na Meneja wa Ofisi za Azam Complex, Sikitu Kilakala, ametoa msaada wa vitu mbalimbali zikiwemo katoni mbili za juisi ya Azam Embe, kiroba cha unga wa sembe, maziwa, mafuta ya kula, pakiti nne za mchele, sabuni ya unga.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz, Mohammed alisema kuwa huo ni mwanzo tu katika kuwafungulia njia wachezaji wenzake kusaidia jamii hususan watoto kama hao ambao hawana msaada.

“Zoezi hili nitaendelea nalo kila mwezi, nimefanya kwa moyo wangu nimehguswa nao sana na wanahitaji msaada kutoka kwetu, kama Mungu amakupa unatakiwa kuwasaidia watu ambao wanahitaji msaada wako, hawawezi kuja lakini unatakiwa kutambua ya kuwa hii ni kazi ya Mungu,” alisema.

Mohammed alisema Mungu amempa kidogo na kudai anatakiwa kuwasaidia watu ambao hawajabarikiwa kuwa nacho kaka hao watoto.

“Umeona hawana sehemu ya kwenda, watoto hawana wazazi, hata kama wako hapa wakihudumiwa na watu, bado watu hao wanahitaji msaada wetu kutoka kwa kama sisi binafsi, kwa hiyo nimeamua kuwasaidia ili wajione kuwa hawajatengwa na dunia.

Na pia nimejisikia ya kuwa kwa kufanya hivi nitakuwa nimewashawishi wachezaji wenzangu kuiga mfano wangu, wachezaji wengi wanatamani kufanya hivi, lakini hawajui ni kwa namna gani wafanye, kwa hiyo hii itawaonyesha njia. Natarajia Mungu ataendelea kunibariki mimi ili kuweza kuwa hapa kila siku na kuwasaidia,” alimalizia Yahaya ambaye amejiunga Azam FC akitokea Aduana Stars ya Ghana.

#WeAreCommunity