KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Aristica Cioaba, ameweka wazi kuwa hana presha yoyote kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi dhidi Yanga na anavyokiona kikosi chake anaamini kitapambana na kuibuka na ushindi.

Mtanange huo utafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.00 jioni, ambapo Azam FC ina morali kubwa kuelekea mtanange huo huku ikiwa imepanga kuendeleza wimbi lake la matokeo mazuri kwenye mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Cioaba ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa amewapanga wachezaji wake kushinda mchezo huo na kusahau matokeo yaliyopita ya kufungwa  kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mbabane Swallows.

“Naiheshimu Yanga ni timu kubwa hapa Tanzania, msimu uliopita walikuwa mabingwa wa ligi hapa Tanzania, naijua vilivyo Yanga, nawaamini vijana sana wataingia uwanjani na kusahau mechi iliyopita ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuanza upya kwa kucheza vizuri na kupata matokeo.

“Napenda kuwaomba msamaha mashabiki wetu na watu wote wanaoiamini klabu hii kwa matokeo tuliyopata kule Swaziland kwa kufungwa mabao 3-0, kabla ya mchezo tulipata matatizo mengi na naliongelea hili kwa kujiamini kwa kusema nini kilikuwa tatizo, nitajaribu kuwafanya wachezaji kusahau mchezo huo na kuweka akili zao katika mchezo huu wa Yanga na mchezo mwingine muhimu kwetu dhidi ya Ndanda (Kombe la FA),” alisema.

Cioaba aliwaomba mashabiki wa Azam FC kujitokeza tena uwanjani na kuendelea kuisapoti timu hiyo huku akiwaambia kuwa sio jambo zuri kuisapoti timu wakati ikipata ushindi tu bali waendelee pia hata pale inapopoteza mchezo.

“Umeona Azam FC katika miezi mitatu hii, imecheza mechi zake zote kwa nguvu na kukusanya pointi nyingi, imepoteza mchezo mmoja tu ambao ni wa Kombe la Shirikisho Afrika, nadhani kila mmoja hapa anatambua mechi kubwa dhidi ya Simba na Yanga, na mimi umakini wangu ni kuwaweka vema wachezaji ili kuwa na moja ya matokeo mazuri, nahitaji kucheza mchezo mzuri na kushinda mechi ya kesho,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana, alisema kuwa anataka kuiona Azam FC hatua kwa hatua ikicheza soka zuri na kupata matokeo mazuri ili kuwavuta tena mashabiki wa timu wajae uwanjani kuwasapoti.

“Mimi nimekuwa hapa kwa miezi mitatu tu, na nimajaribu kufanya kila lililozuri katika kipindi change hiki, kwa sasa nawajua wachezaji wangu wa timu, nalijua soka la hapa Tanzania, napenda kila wiki kuweka mbinu zangu kwa namna ninavyotaka timu hii icheze hapo baadaye.

“Lakini jambo hili halitoshi ndani ya miezi mitatu tu kwa kocha yoyote, lakini hivi sasa kila mmoja anaona Azam FC ilivyobadilika, baadhi ya wachezaji wamebadilika kiuchezaji napenda kuona wanavyokuwa wakija mazoezi na kufanya kwa nguvu, ndani ya mechi wamekuwa wakiheshimu mbinu, hivi sasa wanahitaji kazi zaidi kila wiki na hapo baadaye labda timu hii inaweza kuwa yenye nguvu zaidi na kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi,” alisema.

Aidha Cioaba alisema amekuwa akieleza kila siku kuwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi si mahala pa Azam FC huku akidai timu hiyo inatakiwa kuwa nafasi ya juu zaidi kila mara kutokana na ubora waliokuwa nao.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo, ikiwa na rekodi nzuri ya kutoruhusu wavu wake kuguswa kwenye mechi saba za ligi zilizopita na kuwa ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote wa ligi tokea mwaka huu uanze.

Ushindi wowote kesho wa Azam FC yenye pointi 44 katika nafasi ya tatu, utakuwa unaisogeza zaidi kwenye nafasi ya pili kwani itakuwa imebakisha pointi sita ili iweze kuikamata Yanga, ambayo imejikusanyia 53 mpaka sasa.