KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kimeingia kambini jioni hii katika makao makuu yake ya Azam Complex, tayari kabisa kufanya maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo ujao dhidi ya Yanga.

Mtanange huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utafanyika Jumamosi ijayo katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo Azam FC imejiwekea malengo ya kuibuka na ushindi ili kuzisogelea nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Azam FC inaingia kambini ikiwa na urejeo wa wachezaji wake saba waliokuwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ambao wataungana rasmi na wenzao mazoezini kuanzia kwenye programu ya kesho Alhamisi.

Wachezaji hao ni kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, viungo Himid Mao ‘Ninja’, Frank Domayo ‘Chumvi’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ huku Gadiel Michael, akiwa tayari ameanza rasmi mazoezi na wenzake leo jioni.

Itakumbukwa kuwa katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo zilitoka suluhu, lakini Azam FC imetoka kuichapa Yanga mabao 4-0 wakati ikitwaa Kombe la Mpinduzi Januari mwaka huu visiwani Zanzibar.

Katika msimamo wa ligi hivi sasa, Azam FC inashika nafasi ya tatu ikiwa imejikusanyia jumla ya pointi 44 pungufu ya 11 walizokuwa nazo Simba kileleni, Yanga ni ya pili ikiwa nazo 53.