ULE mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baina ya wenyeji Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC na Ndanda sasa utafanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Aprili 5 mwaka huu saa 1.00 usiku.

Awali mchezo huo ulipangwa kufanyika kati ya Machi 18 na 19 mwaka huu, lakini ulisogezwa mbele kutokana na Azam FC kuwa kwenye majukumu ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi mwaka huu wanaodhaminiwa na kinywaji safi burudani kwa koo lako cha Azam Cola na Benki bora kabisa nchini ya NMB, walitinga robo fainali baada ya kuipiga Mtibwa Sugar bao 1-0 lililifungwa na winga machachari, Ramadhan Singano ‘Messi’.

Ndanda nayo imefika hapo kwa kuichapa The Might Elephant ya mkoani Ruvuma kwa jumla ya mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia suluhu ndani ya muda wa kawaida wa dakika 90, mchezo uliofanyika Uwanja wa Majimaji, mjini Songea.

Hii ni mara ya tatu kwa timu hizo kukutana katika msimu huu wa ligi na mara ya kwanza kwenye michuano hiyo, ambapo katika mechi mbili zilizopita za ligi kila timu imepata ushindi mara moja, Ndanda ikishinda mabao 2-1 nyumbani kwao na Azam FC ikiibuka kidedea kwa bao 1-0 ndani ya Azam Complex.

Mpaka sasa timu mbili zimeshaingia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, Mbao ikiwa imesonga mbele kwa kuichapa Kagera Sugar mabao 2-0 huku Simba nayo ikipenya baada ya kuifunga Madini ya mkoani Arusha 1-0.

Mbali na mechi hiyo ya Azam FC, mtanange mwingine uliobakia utafanyika Aprili 22 mwaka huu kati ya mabingwa watetezi Yanga na Tanzania Prisons, utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshindi wa michuano hiyo iliyorejea msimu uliopita, anatarajia kujishindia kombe pamoja na kitita cha Sh. milioni 50 na kuiwakilisha Tanzania Bara kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.