BEKI kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aggrey Morris, leo jioni ameanza rasmi mazoezi mepesi ya uwanjani baada ya kupata nafuu ya majeraha yake ya mfupa wa paja la kulia.

Morris alipata majeraha hayo wakati Azam FC ikiichapa Mbabane Swallows bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo katikati ya wiki iliyopita alianza na programu ya mazoezi ya ‘gym’ kabla ya leo kuhamia uwanjani.

Beki huyo anarejea wakati Azam FC ikiwa kwenye maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Yanga, utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi ijayo saa 10.00 jioni.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuhusu urejeo wake, Morris alionyesha furaha yake huku akiomba sapoti kwa mashabiki, viongozi na wachezaji wenzake.

“Namshukuru Mungu kwa kuweza kurejea uwanjani kwa sababu mchezaji lengo lake ni kucheza na sio kukaa juu (jukwaani), hamna kitu kibaya kwa mchezaji kama majeraha yakikuandama mara kwa mara yanaweza kukupotezea akili yako yote ya mpira,” alisema.

Aizungumzia mechi Yanga

Morris alizungumzia mchezo ujao dhidi ya Yanga na kusema yupo vizuri kwa ajili ya mchezo huo huku akidai kuwa wamejipanga kushinda mtanange huo.

“Kusema kweli mchezo ni mgumu kwa sababu Yanga ukiangalia ni timu kubwa, naiheshimu, ina wachezaji wazuri imejiandaa kwa sababu ukiangalia wao wanataka ubingwa, ila na sisi tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunawafunga kwa sababu lengo letu sisi ni kushinda kila mchezo unaokuja mbele yetu, tukiwa kama Azam tunauhitaji sana mchezo huu ili kuendeleza katika nafasi ya pili tunayoitarajia,” alisema.

Rekodi ya kutofungwa

Ukiachilia mbali kupoteza mchezo uliopita wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa mabao 3-0 na Mbabane Swallows ya Swaziland, Azam FC mpaka sasa katika mechi saba zilizopita (sawa na dakika 630) za ligi haijaruhusu wavu wake kuguswa na kupoteza mchezo.

Akizungumzia rekodi hiyo, beki huyo mkongwe ambaye ni mmoja wa wachezaji waliocheza muda mrefu ndani ya timu hiyo alisema siri ya mafanikio hayo inatokana na umoja waliokuwa nao katika timu kuanzia kwenye eneo la ulinzi, kiungo na ushambuliaji.

“Wanaolinda si watu wa nyuma tu hata mbele tu kule wanalinda ndio maana tunapata ‘cleansheet’ (kutoruhusu bao), kwangu mimi ni furaha kama beki kupata cleansheet katika mechi saba,” alimalizia.

Hadi anarejea dimbani baada ya kukosekana kwa wiki mbili, Morris amekosa mechi moja tu dhidi ya Mbabane Swallows iliyofanyika mjini Mbabane, wiki moja iliyopita.