BENCHI la Utabibu la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, limeweka wazi taarifa mpya zinazowahusu wachezaji watatu wa timu hiyo, nahodha John Bocco ‘Adebayor’, Aggrey Morris na Stephan Kingue, ambao ni majeruhi.

Wakati Bocco na Kingue wakisumbuliwa na misuli ya nyama za paja, majeraha waliyopata kwenye mchezo dhidi ya Simba, Morris alipata majeraha madogo ya kupata ufa kwenye mfupa wa paja lake la kulia katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mbabane Swallows.

Daktari wa mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu, Mwanandi Mwankemwa, alisema kuwa Morris kwa sasa yupo katika hatua za mwisho za kurejea uwanjani, ambapo anatarajia kuanza rasmi mazoezi na wenzake Jumatatu ijayo.

“Morris yupo katika hatua zake za mwisho za matibabu na mapumziko na Jumatatu ijayo ataanza mazoezi tayari kwa ushindani na mechi zilizobakia za ligi, kwa hiyo kuanzia Jumatatu tutakuwa naye,” alisema.

Bocco Sauzi

Mwankemwa pia alizungumzia majeraha ya Bocco baada ya kufanyiwa uchunguzi nchini Afrika Kusini wakati Azam FC ilipopiga kambi nchini humo kujiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya Mbabane, ambapo amedai kuwa hali yake inaendelea vizuri kwa sasa na anatakiwa kupumzika hadi Aprili 15 mwaka huu atakaruhusiwa kucheza.

“Kingue alichanika msuli wa paja wa mbele ambao kitaalamu tunauita ‘accelerator’ na John Bocco alichanika msuli wa paja wa nyuma ambao tunauita ‘decelerator’, misuli ya paja ya mbele inasaidia mchezaji kwenda kasi zaidi, na misuli ya paja ya nyuma inasaidia mchezaji kupunguza ile kasi.

“Wote walipata matibabu hapa lakini tulipokwenda Afrika Kusini, Bocco alikwenda katika Hospitali ya Muelmed, iliyopo katika mji wa Pretoria katika mtaa wa Pretorious, alionwa na daktari ambaye ni Dr. Bloem Ingelyf, ambaye ni daktari bingwa wa fani hii ya mifupa na akafanyiwa vipimo vya ‘ultrasound’,” alisema.

Aidha alisema mara baada ya vipimo hivyo, Bocco alibainika kuwa hana tena dalili yoyote ya kuchanika misuli wala uwepo wa uwekaji majimaji au buja la damu katika paja na kusisitiza kuwa mshambuliaji huyo kipenzi wa timu hiyo ameanza kupona.

“Lakini daktari bado ametushauri kwamba katika wiki mbili hizi, John Bocco afanye mazoezi madogo madogo na apumzike na katika wiki ya tatu John Bocco ndio aanze kufanya mazoezi ya nguvu kwa hiyo inamaanisha ya kwamba John Bocco ataweza kuanza kucheza soka la ushindani kuanzia Aprili 15,” alisema.

Kingue je?    

Kuhusu kiungo Kingue, daktari huyo bingwa alisema kuwa kwa upande wake ilishindikana kubakia Afrika Kusini kutokana na viza yake ya kubakia huko kuwa imeisha, ambapo kwa sasa mipango inafanyika ya Kingue kurejea nchini humo.

“Ilitakiwa tubakie naye Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa vipimo kama ilivyokuwa kwa Bocco, lakini viza yake ya Cameroon ilisumbua, kwa hiyo taratibu zinafanywa hivi sasa na uongozi wa timu ya Azam FC ili wiki ijayo Stephan naye aweze kwenda kufanyiwa vipimo,” alisema

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola kinachoburudisha mwili na Benki bora nchini ya NMB, tokea jana jioni ilianza rasmi mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Yanga, utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili Mosi mwaka huu.