KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, jioni ya leo imeanza rasmi mazoezi ya kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Yanga.

Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utafanyika Aprili Mosi mwaka huu ndani ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kikosi hicho kimeanza mazoezi huku kikiwakosa nyota wake saba waliokuwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ambao ni kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Gadiel Michael.

Viungo ni Nahodha Msaidizi Himid Mao, Frank Domayo na Salum Abubakar, ambao wanajiandaa na mechi mbili za kimataifa za kirafiki dhidi ya Botswana (Machi 25) na Burundi (Machi 28).

Mara ya mwisho Azam FC kukutana na Yanga, ilikuwa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, ilipopata ushindi wa kihistoria dhidi ya wanajangwani hao baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Katika mchezo wa raundi ya kwanza ya ligi, timu hizo zilitoka suluhu huku ikishuhudiwa Azam FC ikitawala mchezo na kukosa nafasi nyingi za kufunga mabao.

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, alisema kuwa vijana wake wamerejea mazoezi wakiwa na ari nzuri baada ya mapumziko ya siku mbili.

“Leo tumeanza mazoezi mepesi, kesho tena tutaendelea na mazoezi mengine kwa ajili ya kujiwinda na mchezo dhidi ya Yanga, wachezaji wetu sana wapo timu ya Taifa, wawili wanamjeruhi kidogo na ndio maana umeona namba ya wachezaji ipo kidogo leo ikiwa imepwaya,” alisema.

Cheche alizungumzia kama wanaweza kuathirika kwenye maandalizi yao baada ya kuwakosa wachezaji saba, ambapo amedai kuwa kwa kiasi fulani wataathirika lakini watatafuta namna gani ya kukabiliana na suala hilo.

“Kitu chochote kinachofanywa kwa umoja kinakuwa ni kizuri zaidi sasa tunapokuwa tumegawanyika kidogo kuna athari fulani ipo, lakini tutajaribu kutafuta namna jinsi gani tutaikabili kwa sababu ukiacha hizi siku chache ambazo watakuwa hawapo pamoja, hapo nyuma nafikiri walikuwa pamoja.

“Tuombe Mungu wanapokwenda huko timu ya Taifa wasipate majeraha katika kuelekea mchezo wetu dhidi ya Yanga, mchezo utakuwa mgumu na ni mapema mno kuuongelea kwa sababu ndio tumeanza maandalizi leo na bado tuna siku tano za kujiandaa,” alisema.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola pamoja na Benki bora ya NMB, itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na pointi zake 44 katika nafasi ya tatu, ikizidiwa pointi 11 na kinara Simba aliyejikusanyia 55 huku Yanga ikijizolea 53 kwenye nafasi ya pili.