KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeshindwa kutinga kwenye raundi ya mwisho ya mtoano ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa na Mbabane Swallows mabao 3-0 jana jioni katika mchezo wa marudiano uliofanyika Uwanja wa Taifa wa Somhlolo, Swaziland.

Kwa ushindi huo wa Swallows, unaifanya kufuzu kwa raundi ijayo kwa jumla ya mabao 3-1 kufuatia ushindi wa bao 1-0 iliyoupata Azam FC katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Azam FC ilikianza vizuri kipindi cha kwanza kwenye dakika 35 za mwanzo kwa kufanikiwa kuwabana wapinzani wao huku ikitengeneza nafasi kadhaa zilizoshindwa kutumiwa na mshambuliaji wake, Yahaya Mohammed, ambaye alipoteza nafasi muhimu za kuifungia mabao timu hiyo katika vipindi vyote.

Mbabane Swallows ilijipatia bao lake la kwanza dakika ya 40 kupitia kwa mshambuliaji wake, Sandile Ndzinisa na kipindi cha kwanza kumalizika kwa uongozi wa bao hilo moja, ambalo lilifanya matokeo ya jumla kuwa 1-1 kutokana na ushindi wa bao 1-0 wa Azam FC katika mchezo wa kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kufanya mabadiliko kwa kuimarishwa eneo la ushambuliaji baada ya kupumzishwa Ersato Nyoni, aliyekuwa akicheza kiungo mkabaji na kuingia mshambuliaji Shaaban Idd.

Dakika mbili tu baada ya kuingia, Shaaban alijaribu kuipa bao la kusawazisha Azam FC baada ya kuingia kwenye eneo la hatari na kupiga shuti zuri lililopanguliwa na kipa wa Mbabane, Sandile Ginindla na Yahaya kushindwa kuumalizia mpira baada ya kuukosa.

Mbabane walijipatia mabao yao mawili ya mwisho yaliyokamilisha ushindi wao kupitia kwa Wonder Nhleko dakika ya 66 na Sandile Hlatjwayo dakika 74 na licha ya Azam FC kufanya mabadiliko ya kuwaingiza Samuel Afful na Joseph Mahundi, ilishindwa kupindua matokeo hayo.

Vurugu zajitokeza

Kabla ya kuanza mchezo huo, wakati kikosi cha Azam FC kikiwasili uwanjani, mashabiki wa Mbabane kwa kushirikiana na polisi wa Swaziland walishirikiana kuifanyia vurugu timu hiyo kwa kuizuia isiteremke ndani ya basi.

Hali hiyo ilisababisha Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, kusukumwa, kupigwa na kuangushwa na polisi pamoja na mashabiki hao wakati akijaribu kupigania haki ya Azam FC kwa kushirikiana na maofisa usalama walioongozana na timu hiyo.

Maofisa usalama wa Azam FC waliokabiliana na mashabiki kuzima vurugu hizo waliongozwa na Kondo Idd almaarufu kama Karume, Juma Mdunguma, Kheri Mzozo, Edward Msimbe na Biggie Papa.

Katika hatua nyingine, Azam FC ililazimika kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo baada ya kupuliziwa dawa kali, hali iliyoilazimu kubadilisha nguo kwenye basi za kuvaa katika njia ya kuingia vyumbani.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaanza rasmu safari ya kurejea Tanzania kesho Jumatatu saa 6.15 kikiondoka katika Uwanja wa Ndege ya Kimataifa wa OR Tambo nchini Afrika Kusini kikipitia nchini Kenya kabla ya kutua jijini Dar es Salaam saa 3.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Bruce Kangwa, Daniel Amoah, Yakubu Mohammed, Erasto Nyoni/Shaaban Idd dk 46, Salum Abubakar, Himid Mao, Yahaya Mohammed/Joseph Mahundi dk 84, Frank Domayo, Ramadhan Singano/Samuel Afful dk 69