KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kimerejea jijini Dar es Salaam usiku huu kikitokea nchini Swaziland kilipoenda kucheza mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mbabane Swallows na kufungwa mabao 3-0 juzi.

Azam FC iliyotolewa kwenye michuano hiyo kwa jumla ya mabao 3-1, ilianzia safari yake saa 6.15 mchana jijini Johannesburg kwa usafiri wa Ndege ya Shirika la Kenya (KQ) ikipitia nchini Kenya kabla ya kuunganisha ndege iliyowafikisha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl Julius Nyerere (JNIA) ilipotua saa 3.00 usiku.

Mara baada ya kuwasili wachezaji wa timu hiyo wamepewa mapumziko ya siku mbili hadi Alhamisi ijayo itakapoanza tena mazoezi saa 10.00 jioni kujiandaa na mechi zinazokuja za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Wachezaji saba wa Azam FC waliochaguliwa kwenye kikosi kipya cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ nao wamepewa ruhusu ya kujiunga na kambi ya timu hiyo leo Jumanne.

Wachezaji hao ni kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, viungo Himid Mao ‘Ninja’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Frank Domayo ‘Chumvi’.

Vita yahamia VPL, FA Cup

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, ameweka wazi kuwa wameshasahau yaliyopita na nguvu zao kwa sasa wanazielekeza katika michuano ya Ligi Kuu na Kombe la FA, ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.

“Sipendi kuongelea matatizo yaliyotokea kabla ya mchezo (vurugu), nitaongelea kilichotokea dakika 45 za kipindi cha kwanza, timu ilitengeneza nafasi mbili za wazi na kama unavyojua kupoteza nafasi adimu kwenye mechi ya ugenini ni balaa, hakika safu ya ushambuliaji ilituangusha,” alisema.

Aidha Cioaba alisema kuwa moja ya mambo watakayoendelea kufanya ni kuhahakisha wanakusanya pointi za kutosha kwenye ligi na kutinga hatua ya fainali ya Kombe la FA ikiwemo kutwaa taji hilo.

“Bado tunanafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani, nitawapanga kuwajenga wachezaji kusahau yaliyopita, tuna mchezo mwingine mkubwa ujao dhidi ya Yanga hivyo tunahitaji kuingia kwenye mchezo huo tukiwa vizuri, tumeshaingia hatua ya robo fainali ya FA, sasa ni wakati wa kuingia nusu fainali kwa kuifunga Ndanda kisha kuingia fainali na kutwaa kombe,” alisema.

Wakati ikiwa imebakisha mechi sita kuweza kumaliza ligi, Azam FC imejikusanyia jumla ya pointi 44 katika nafasi ya tatu, ikizidiwa pointi 11 na kinara Simba anayeongoza, Yanga ni ya pili ikiwa imejizolea 53.