WAKATI ikiwa imebakia siku moja tu kumenyana na Mbabane Swallows, Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, amejinasibu ya kuwa anakiamini kikosi chake kitapata matokeo mazuri kesho Jumapili katika mchezo huo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Mchezo huo wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo, utafanyika katika Uwanja wa Taifa wa Somhlolo, mjini Mbabane, Swaziland utakaoanza saa 10.30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Azam FC kuelekea mchezo huo, imepiga kambi jijini Pretoria, Afrika Kusini tokea Jumatano iliyopita na inatarajia kuelekea nchini Swaziland leo Jumamosi wakiwa na morali kubwa ya kupata matokeo mazuri.

Cioaba mara baada ya mazoezi ya jana jioni ameuambia mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa kikosi chake kipo vizuri kuelekea mchezo huo huku akiwaomba wachezaji wake kuonesha hali ya kupambana uwanjani ili kufanikisha ushindi na kusonga mbele.

“Jana (juzi) ilikuwa ni mazoezi ya kwanza na leo (jana) ni ya pili, nimewaangalia wachezaji wangu wako vizuri leo wakiwa na hamasa na hili ni jambo zuri, kesho (leo) nina nafasi ya kufanya mazoezi ya mwisho hapa ambayo ndio yatakuwa ya mwisho kuelekea mchezo wa Jumapili (kesho).

“Baada ya mazoezi tutasafiri kuelekea Swaziland na Jumapili nataka wachezaji wangu wote wafuate ujumbe wangu waingie uwanjani na kupambana kwa ajili ya kufuzu kwa raundi ijayo,” alisema kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana.

Anautazamaje mchezo huo

Akizungumzia mchezo huo, Cioaba alisema kuwa utakuwa ni mchezo tofauti kidogo kwa kuwa wanacheza ugenini huku akiwa tayari amefanya kazi na wachezaji wake kwa kuwapa mbinu tofauti za namna ya kuukabili.

“Unapocheza ugenini unatakiwa kubadilisha baadhi ya vitu kwenye mbinu, nitafanya kazi na wachezaji kuhusiana na hilo wachezaji wamekuwa wakinisikiliza, nimeona leo wanavyonisikiliza, nawaamini wachezaji wangu, namuamini Mungu wangu nitapata matokeo mazuri na klabu ya Azam itashinda mchezo na kufuzu kwenye hii michuano.

“Ni jambo muhimu kwa timu baada ya kukaa kipindi kirefu bila kupoteza mchezo, timu imekuwa ikipanda hatua kwa hatua kila wiki kutokana na hilo moyoni mwangu naiamini timu Jumapili itapata matokeo mazuri,” alisema.

Kuziba mapengo

“Nitawakosa baadhi ya wachezaji wangu, lakini nimeshaongea na wachezaji wote kuwa timu ina wachezaji wengi ambao wanaweza kuingia na kucheza kwenye nafasi hizo, wanahitaji kupigania majina yao, kupigania nafasi, kupigania timu kwa ajili ya kuweza kupata matokeo mazuri, ni nafasi kubwa kwa mchezaji mwingine mpya kuingia uwanjani kwa mimi kumpa nafasi, ninaamini na kujiamini kuwa wachezaji wangu wote wataingia uwanjani na kuisaidia timu ipate matokeo mazuri,” alisema.

Matokeo mazuri yatakayoivusha

Baada ya kuondoka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa awali, Azam FC inahitaji kupata ushindi wowote au sare yoyote ili kuweza kusonga mbele kwa hatua ya mwisho ya mtoano (play off).

Moja ya silaha kubwa za Azam FC katika kuhakikisha inasonga mbele ni kuhakikisha inapata bao la ugenini, ambalo litazidi kuongeza mlima kwa wenyeji hao kuweza kupenya kwa raundi ijayo.

Azam FC ikipata bao la ugenini basi kimahesabu ya kusonga mbele itakuwa inajiweka vizuri, kwani hata kama wenyeji hao watapata ushindi wowote wa tofauti ya bao moja kuanzia 2-1 na kuendelea, basi moja kwa moja Azam FC itakuwa inanufaika kwa kupata nafasi ya kupiga kupitia bao la ugenini.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu, wakipita raundi hiyo watakuwa wameelekea kwenye hatua ya mwisho ya mtoano, ambayo mwezi ujao watapangwa kukutana na moja ya timu 16 zilizotolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.