KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetua salama nchini Afrika Kusini jana jioni huku ikiwa na morali kubwa ya kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mbabane Swallows.

Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Taifa wa Somhlolo, nchini Swaziland Jumapili hii saa 10.30 kwa saa Afrika Mashariki, ambapo Azam FC  itaingia dimbani ikiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 walioupata katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam, bao lililofungwa na winga Ramadhan Singano ‘Messi’.

Kikosi hicho kilichopiga kambi ya siku tatu Afrika Kusini katika Hoteli ya Acardia, jijini Pretoria, kitafanya maandalizi yake yote nchini humo kabla ya kuelekea Swaziland Jumamosi asubuhi kwa ajili ya mchezo huo.

Msafara wa Azam FC unaongozwa na Mwenyekiti Nassor Idrissa ‘Father’, Mlezi wa timu, Jamal Bakhresa, aliyeongozana na baadhi ya viongozi wengine Meneja Mkuu, Abdul Mohamed, Meneja wa timu, Phillip Alando huku Mtendaji Mkuu Saad Kawemba akitarajia kuwasili muda wowote kuanzia sasa kuungana na kikosi hicho, pia wengine waliosasili ni viongozi wakuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Makamu wa Rais, Wallace Karia na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, James Mhagama.

Akizungungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz Mwenyekiti wa timu hiyo, Nassor Idrissa, alisema wanaelekea kwenye mchezo huo wakiwa na nia ya dhati ya kuhakikisha Azam FC inapata matokeo mazuri kwa ajili ya kusonga mbele kwa raundi ijayo.

“Kwanza tunamshukuru Mungu kwa kufika salama hapa, ilikuwa ni safari ndefu, tumekuja viongozi, timu kwa maana ya wachezaji na makocha, tumefika hapa Afrika Kusini kwa ajili ya kuweka kambi ya siku nne hapa mjini Pretoria na tutaondoka Jumamosi kuelekea Swaziland kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Mbabane Swallows,” alisema.

Father pia alizungumzia hali za wachezaji wao kuelekea mchezo huo, akisema kuwa kisaikolojia wapo vizuri na shauku kubwa ya kupambana na kuifanya Azam FC isonge mbele kwa raundi ijayo.

“Wachezaji wanashauku kubwa, kazi iliyobaki ni ya mwalimu kuwafundisha mbinu za kuja kupambana, sisi kama viongozi tumejitahidi kwa uwezo wetu kama unavyoona tumewaleta hapa siku nne kabla ya mchezo wawe karibu na jiji hili la kule Mbabane na hali ya hewa zikilingana, na kingine watakuwa wametulia kwa ajili ya maandalizi mazuri,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Mpira wa miguu ni mchezo wa dakika 90, tungeshinda bao moja, tungeshinda mbili, tumeona wenzetu Ulaya juzi (PSG v Barcelona) mfano mmoja walishinda nne nyumbani (PSG), lakini wakatolewa ugenini, hivyo unapocheza mchezo mwingine ni jambo tofauti, tumesahau yaliyopita ile ni kama dakika 90 ambazo ni kipindi cha kwanza kimeisha.

“Mpira haujamalizika tuna dakika 90 nyingine kucheza nyumbani kwao, lolote linaweza kutokea kwa sababu kucheza nyumbani sio hoja lakini hoja ni namna ulivyojipanga na mbinu zako ili uweze kupata ushindi.”

Bosi huyo wa matajiri hao wa Azam Complex, alimaliza kwa kuwaomba mashabiki waendelee kuwasapoti kwa kuwashangilia huku akiomba pia dua zao kuelekea mchezo huo.

“Waendelee bado mchezo haujamalizika, ndio kwanza dakika 90 za kwanza bado dakika 90 nyingine zinatusubiri, kwa hiyo nguvu yao, dua zao, hamasa zao, kila kitu ambacho wanacho kuweza kuisapoti timu wakiendeleze,” alimazia.

Azam FC inayotakiwa kupata sare yoyote au ushindi wowote ili kusonga mbele, inatarajia kufanya mazoezi ya kwanza jijini hapa leo Alhamisi jioni.