KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, usiku huu imemaliza mazoezi ya mwisho kabla ya leo Jumatano asubuhi kuanza safari ya kuelekea kwenye mchezo wake wa marudiano wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mbabane Swallows, utakaofanyika Uwanja wa Somhlolo, mjini Mbabane, Swaziland Jumapili hii Machi 19.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi mwaka huu, wanaonolewa na Kocha Mkuu Aristica Cioaba raia wa Romania, wataondoka na Ndege ya Shirika la Kenya Airways.

Azam FC tokea imalize mchezo wake wa kwanza uliofanyika Jumapili, mara moja Jumatatu jioni ilianza maandalizi kwa ajili ya kipute hicho cha marudiano, ambapo inaenda huko ikiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0.

Morali ya kikosi hicho iko juu kuelekea mchezo huo na Azam FC inahitaji sare yoyote au ushindi wowote ili kuweza kusonga mbele kwa raundi ya mwisho ya mtoano (play off) na huko itakutana na moja kati ya timu 16 zitakazokuwa zimetoka kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza na mtandao huu www.azamfc,co,tz Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, alisema kuwa maandalizi yao kuelekea mchezo huo yapo vizuri huku akigusia kuwa wanaenda huko wakiwa na changamoto kadhaa ya kwanza ikiwa ni kuhakikisha wavu wao hautikiswi.

“Maandalizi yako vizuri vijana wote wanafuraha, wanaari na morali ya kuhahakisha tunasonga mbele katika raundi inayofuata, tunaenda na changamoto kadhaa, ya kwanza kuhahakisha wavu wetu hautikiswi, kama hatufungi basi tusifungwe,” alisema.

Cheche alisema kuwa watahakikisha wanalinda ushindi walioupata nyumbani na kufanya mashambulizi kwenye lango la wapinzani.

“Tutaenda kufanya kazi ya uhakika, lakini huku nyumbani tunawaomba Watanzania watuombee dua na vilevile waendelee kutusapoti na sisi tutahakikisha tunawawakilisha vema ili kuipa hadhi nchi yetu,” alisema.

Naye Nahodha Msaidizi wa Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, alizungumza kwa upande wa wachezaji wenzake akisema kuwa kwa asilimia kubwa wao wako vizuri kuelekea mchezo huo huku akisisitiza kuwa wanaenda huko kulinda ushindi walioupata nyumbani.

“Maandalizi yako poa, asilimia kubwa ya wachezaji wako vizuri isipokuwa baadhi ya wachezaji wanauchovu tu baada ya mchezo wa kwanza, naamini kesho kila mtu atakuwa poa, kitu cha kwanza ni ushindi, japo ni bao moja lakini hatukuruhusu bao.

“Tunaenda tuna faida na tuna goli na hatujaruhusu goli, kwa hiyo nafikiri mechi inayokuja kazi yetu si kubwa sana japo ni kubwa pia, huwezi kusema tumemaliza au hatujamaliza, tunakazi kubwa ya kufanya kule ya kulinda ushindi wetu tulioupata hapa nyumbani ili tuweze kusonga mbele,” alisema.

Tafadhali tunakuomba uendelee kufuatilia mtandao huu na mitandao yetu ya kijamii ya facebook (Azam FC) na ule wa Instagram (azamfcofficial) ili kupata habari zetu mbalimbali.