NYOTA saba wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, wamejumuishwa kwenye kikosi kipya cha wachezaji 26 wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kilichotangazwa jana na Kocha Mkuu, Salum Mayanga.

Kwa idadi hiyo ya wachezaji, inaifanya Azam FC kuwa miongoni mwa timu mbili zilizotoa wachezaji wengi katika kikosi hicho, ikilingana na Simba ambayo nayo imetoa wachezaji saba, huku kwa upande wa Yanga wakiitwa wanne tu.

Katika kikosi hicho kitakachoingia kambini Machi 19 kujiandaa michezo ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), kina wachezaji wawili kutoka Mtibwa Sugar, huku Kagera Sugar, Mwadui na Ruvu Shooting, zikitoa mmoja kila moja.

Wachezaji wa Azam FC walioitwa ni kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni na Gadiel Michael, aliyeitwa kwa mara ya kwanza, viungo Himid Mao ‘Ninja’, pamoja na Frank Domayo ‘Chumvi’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambao wamerejeshwa kwenye kikosi hicho baada ya kukosekana kwa muda mrefu.

Gadiel afurahishwa

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya kuitwa kwa mara ya kwanza kikosi hicho, Gadiel alionyesha kufurahishwa huku akimshukuru Kocha Mayanga kwa kutambua uwezo wake.

“Ninafuraha sana, nimechezea timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 huko nyuma, najisikia vizuri kuitwa kwenye kikosi cha wakubwa, namshukuru kocha kwa kutambua uwezo wangu, naahidi kama ninavyofanya Azam FC nitaendelea kupambana kwa ajili ya kupigania namba kikosini,” alisema.

Beki huyo kinda wa kushoto mwenye kasi ya kupanda kusaidia mashambulizi na kushuka kuimarisha ulinzi, alichukua fursa hiyo kuipongeza Azam FC kwa kumwamini na kuahidi kuendelea kuipigania timu hiyo ili kufikia kwenye malengo waliyojiwekea.

Kwa ujumla kikosi alichoteua Mayanga kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Azam), Deogratius Munishi ‘Dida’ (Yanga) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).

Mabeki; Shomary Kapombe (Azam), Hassan Kessy (Yanga), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba), Gardiel Michael (Azam), Andrew Vincent (Yanga), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba) na Erasto Nyoni (Azam FC).

Viungo ni Himid Mao (Azam), Jonas Mkude (Simba), Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Azam), Said Ndemla (Simba), Frank Domayo (Azam), Muzamiru Yassin (Simba), Simon Msuva (Yanga), Shiza Kichuya (Simba), Farid Mussa (CD Tenerife, Hispania) na Hassan Kabunda (Mwadui FC).

Washambuliaji ni Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (AFC Eskilstuna, Sweden), Ibrahim Hajib (Simba), Mbarak Yussuf (Kagera Sugar) na Abdulrahman Mussa (Ruvu Shooting).