KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeutumia vema uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex baada ya kuichapa Mbabane Swallows ya Swaziland bao 1-0, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Shujaa wa Azam FC leo katika mchezo huo wa ruandi ya kwanza ya michuano hiyo, alikuwa ni winga wa timu hiyo Ramadhan Singano ‘Messi’, aliyefunga bao pekee dakika ya 84 akitumia vema pasi ya Shaaban Idd.

Bao hilo linamfanya Singano kuwa ndiye mchezaji aliyefunga la kwanza la Azam FC kwenye michuano hiyo msimu huu na mwaka jana akiwa amefunga la mwisho wakati Azam FC ikiichapa Esperance mabao 2-1, yote akitupia ndani ya Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC ilitangulia kuanza kulisaka lango la Mbabane na katika dakika ya pili tu, mshambuliaji Yahaya Mohammed alikosa nafasi ya wazi akiwa anamchungulia kipa wa timu hiyo kufuatia kupiga kichwa kilichopaa juu ya lango.

Dakika ya 36, kiungo wa Azam FC Salum Abubakar, alipiga shuti zuri lilimlazimu kipa wa Mbabane kuutema mpira kabla ya kuuwahi na kuudaka tena.

Mchezo huo uliokuwa mkali na wa aina yake kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, ilishuhudiwa timu zote zikishindwa kutambiana kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili Azam FC ilikianza kwa kasi na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga mabao, lakini umakini ulikosekana kwenye eneo la ushambuliaji lililokuwa likiongozwa na Yahaya.

Dakika ya 59, Azam FC ilipata pigo baada ya kuumia kwa beki wake kisiki Aggrey Morris, ambaye alipata maumivu ya nyama za paja mara baada ya kupiga shuti kufuatia mpira wa adhabu ndogo aliptanguliziwa na Himid Mao na nafasi yake ilichukuliwa na Daniel Amoah.

Mabadiliko ya Azam FC dakika ya 75 ya kuingia Khamis Mcha na kutoka Yahaya, yaliimarisha eneo la ushambuliaji la Azam FC na hatimaye shambulizi lililofanywa dakika 84 lilizaa bao pekee lilofungwa na Singano.

Kuelekea mwishoni mwa mchezo huo, mshambuliaji wa Azam FC Shaaban Idd, alishindwa kuipatia bao la pili timu hiyo baada ya kubaki na kipa lakini shuti alilopiga lilimlenga kipa, nafasi hiyo alitengenezewa kiufundi na Mcha.

Ushindi huo unazidi kuimarisha rekodi ya Azam FC kwenye uwanja huo tokea ianze kuutumia kwenye michuano hiyo ya Afrika, ambapo katika mechi tano ilizocheza imeshinda zote kwa ushindi wa asilimia 100.

Katika hatua nyingine imjiongezea rekodi yake bora tokea mwaka huu uanze, ambapo huo ulikuwa ni mchezo wa 16, ikiwa haijafungwa hata mmoja na kuruhusu wavu wake kuguswa mara moja, na kwenye mechi nane zilizopita haijafanikiwa kuruhusu wavu wake kuguswa.

Mara baada ya Azam FC kumaliza mchezo huo, kesho jioni kinatarajia kuanza maandalizi ya mchezo wa marudiano utakaofanyika mjini Mbabane, Swaziland Machi 19 mwaka huu.

Katika mchezo huo wa marudiano, Azam FC ili ivuke kwa hatua ya mwisho ya mtoano (play off) inahitaji ushindi wowote au sare yoyote.

Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Bruce Kangwa, Aggrey Morris/Amoah dk 59, Yakubu Mohammed, Himid Mao (C), Frank Domayo, Salum Abubakar, Joseph Mahundi/Shaaban dk 54, Yahaya Mohammed/Mcha dk 75, Ramadhan Singano