UMESHANUNUA tiketi yako? Kama hujafanya hivyo bado haujachelewa, unachotakiwa kufanya hivi sasa ni kuingia kwenye mtandao wa Kampuni ya Selcom na kujinunulia tiketi yako mapema na kuweza kupata nafasi ya kuishuhudia Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, ikivaana na Mbabane Swallows ya Swaziland.

Mchezo huo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, utafanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Jumapili hii saa 1.15 usiku, ambapo tiketi hizo za elektroniki zilizoanza kuuzwa tokea jana Jumatano zinapatikana kwa Sh. 10,000 kwa mashabiki wa V.I.P A, Sh. 5,000 kwa V.I.P B huku wale mashabiki wa majukwaa ya mzunguko wakilipia Sh. 3,000.

Kuelekea mchezo huo, mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz umefanya mahojiano maalumu na Nahodha Msaidizi wa timu hiyo, Himid Mao ‘Ninja’, ambaye amesema kuwa wanaendelea vema na maandalizi kuelekea mchezo huo huku akitoa wito kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti siku hiyo.

“Maandalizi yako vizuri, ikizingatiwa ni mechi nzuri halafu pia sisi tunarekodi nzuri kwenye uwanja wetu, lakini hiyo haitufanyi tubweteke tutajiandaa vizuri ili tuweze kushinda mchezo,” alisema.

Kiu ya Azam FC makundi

Kwa muda mrefu tokea Azam FC ianze kushiriki michuano hiyo ya Afrika kuanzia mwaka 2013, imekuwa na kiu kubwa ya kuingia hatua ya makundi lakini imekuwa ikishindwa kufanya hivyo.

Akizungumzia ujio wao safari hii, Himid amedai kuwa huu ni mwaka wao wa kuweza kutimiza malengo hayo ya klabu pamoja na yale ya mchezaji mmoja mmoja kwa kufikia mafanikio.

“Nafikiri klabu kama klabu imeshaweka malengo yake na mwalimu aliyepo naye ana malengo yake na sisi kama wachezaji tunamalengo pia kwa sababu sio kitu kizuri kama kila siku unacheza halafu hufanikiwi, kwa hiyo naamini hivi sasa ni wakati wetu wa sisi kutimiza lengo la klabu na la mchezaji mmoja mmoja, anataka kucheza mechi nyingi itamsaidia yeye katika malengo yake ya baadaye,” alisema.

Tahadhari na mabao

Himid aliongeza kuwa: “Kuhusu kushinda ni kitu muhimu kwa timu, timu inataka kushinda lakini tunatakiwa kuwa na tahadhari ili tushinde lazima tujiangalie mara mbili mbili, tunaendaje kushinda?, lakini ukiangalia rekodi yetu ya mechi zilizopita ni nzuri kidogo na inaridhisha kwa hiyo tukiongeza jitihada kidogo tunaweza kupata ushindi mzuri kabisa.

“Kwa sababu katika mechi hizi za mtoano kinachoangaliwa si kushinda tu bali unashindaje?, unaweza ukashinda 1-0 hapa ikawa tatizo, kwa hiyo tutajitahidi kushinda goli nyingi na kutoruhusu kufungwa bao lolote kwa ajili ya mechi inayofuata,” alisema.

Ujumbe kwa mashabiki

Kiungo huyo wa kimataifa wa Tanzania, aliwapa ujumbe mmalumu mashabiki akiwaambia wajitokeze kwa wingi kuwashangilia huku akidai kuwa kuja kwao kwa idadi kubwa kutawapa nguvu zaidi uwanjani ya kupata matokeo mazuri.

“Wao waje kwa wingi kutusapoti, watakapokuja kwa wingi watatupa sisi nguvu wao wana sehemu yao kwenye timu hii kwa hiyo watakapokuja kwa wingi kutusapoti na sisi tutafanya vizuri na tutarudisha ushindi kwao,” alisema.

Mara baada ya mchezo huo wa kwanza, Azam FC inatarajia kurudiana na timu baada ya wiki moja katika mchezo utakaopigwa mjini Mbabane kwenye Uwanja wa Taifa wa Somhlolo Machi 19 mwaka huu na mshindi wa jumla atasonga mbele kwa hatua ya mwisho ya mtoano ‘play off’ kabla ya kutinga hatua ya makundi.