ZIMEBAKIA siku nne kabla ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, haijavaana na Mbabane Swallows kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex Jumapili hii saa 1.15 usiku.

Kikosi cha Azam FC kimeshaanza maandalizi rasmi tokea Jumatatu iliyopita kujiandaa na mtanange huo, ambao unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini.

Tayari tiketi za mchezo huo zimeshaanza kuuzwa leo Jumatano kwa mfumo wa kielektroniki kupitia mtandao wa Kampuni ya Selcom, ambao pia ndio wanauza tiketi za aina hiyo kwenye Uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru.

Viiingilio hivyo ni vya kawaida sana na vipo katika makundi matatu tofauti; kiingilio cha chini kikiwa ni Sh. 3,000 kwa majukwaa ya mzunguko, V.I.P B kitakuwa ni Sh. 5,000 na V.I.P A wakilipia Sh. 10,000.

Kuelekea mtanange huo, leo tunaangalia rekodi ya Azam FC tokeo ilipoanza kushiriki michuano ya Afrika, mwaka huu ikiwa ni mara ya tano mfululizo tangu iliposhiriki mara kwanza mwaka 2013 kihistoria baada ya kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2011/2012.

Mwaka 2013 (Kombe la Shirikisho)

Tokea ianze kushiriki michuano ya Afrika mwaka 2013, ikianzia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC imekuwa na rekodi nzuri ya kutumia vema uwanja wake wa nyumbani (Azam Complex) ikiwa haijawahi kutoa sare au kufungwa katika uwanja huo.

Ikiwa inashiriki kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya Afrika, mwaka 2013 ililazimika kutumia Uwanja wa Taifa kama uwanja wa nyumbani katika mechi zake za Kombe la Shirikisho Afrika, kutokana na wakati huo Uwanja wa Azam Complex kutokidhi vigezo vya kuchezewa mechi za Kimataifa.

Azam FC ilianza vema kwa mechi yake ya kwanza ya nyumbani, ikiichapa Al Nasri ya Juba, Sudan Kusini mabao 3-1 huku kiungo Abdi Kassim ‘Babi’ akiandika rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuifungia timu hiyo bao la kwanza kwenye michuano ya Afrika.

Rekodi nyingine iliweza kuandikwa na winga Khamis Mcha, katika mchezo wa ugenini nchini Sudan Kusini ambapo Azam FC ilishinda 5-0 na Mcha kuwa mchezaji wa kwanza wa timu hiyo kufunga mabao matatu ‘hat-trick’ katika michuano hiyo na hivyo Azam FC kusonga mbele kwa jumla ya mabao 8-1.

Azam FC ilipangiwa kukutana na Barrack Young Controller katika raundi ya kwanza, ikianzia ugenini jijini Monrovia kuitandika timu hiyo mabao 2-1, kabla ya kutoa suluhu nyumbani, na raundi ya pili ikakutana vigogo wa Tunisia, FAR Rabat ikitoka suluhu tena nyumbani kabla ya kufungwa 2-1 ugenini na kutolewa.

Kwenye mchezo huo wa ugenini, ilishuhudiwa nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, akikosa mkwaju wa penalti dakika za mwisho ambao kama angeufunga ungeweza kuipeleka mbele timu hiyo na kutinga hatua ya mwisho ya mtoano ‘play off’ kabla ya kuingia katika makundi.

Mwaka 2014 (Kombe la Shirikisho)

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu, waliendelea kujidhatiti na kumaliza tena kwenye nafasi ya pili katika ligi msimu wa 2012/2013 na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam FC safari hiyo ikaingia na gia mpya kwenye michuano hiyo na ikiandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza hapa nchini kutumia uwanja wake wa nyumbani (Azam Complex) katika michuano ya Kimataifa.

Wakati mwaka 2014 ikianza kutumia uwanja wake huo kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo, Azam FC ikaanza raundi ya awali kwa kuichapa Ferroviario da Beira 1-0 nyumbani, kabla ya kutolewa ugenini kwa kufungwa 2-0, katika mchezo ambao uliathiriwa na mvua iliyoharibu uwanja ambao uliweka madimbwi ya maji hali iliyoharibu ladha ya mpira.

Mwaka 2015 (Ligi ya Mabingwa Afrika)

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola na Benki bora ya NMB, ikapiga hatua kubwa msimu wa 2013/2014 baada ya kutwaa ubingwa wa kwanza wa ligi kwa rekodi ya bila kupoteza mchezo wowote, hali iliyoiwashia taa ya kijani ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015.

Ikishiriki kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika, Azam FC ilipangiwa kukutana na moja ya vigogo barani Afrika, El Merreikh ya Sudan na kama kawaida ikaweza kuutumia vema uwanja wake wa nyumbani kwa kuwachapa vigogo wao mabao 2-0, yaliyowekwa wavuni na Didier Kavumbagu na nahodha Bocco, ambayo alifunga bao kichwa kwenye mpira wake wa kwanza kugusa wakati akiingia kutokea benchini.

Lakini Azam FC haikuwa na bahati kwa mara nyingine mwaka huo ya kusonga mbele, baada ya kutolewa ugenini kwa kufungwa mabao 3-0.

Mwaka 2016 (Kombe la Shirikisho)

Kwa mara ya nne mfululizo mwaka jana, Azam FC iliweza kushiriki michuano ya Afrika baada ya kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika kufuatia kushika nafasi ya pili kwenye ligi.

Safari hii, Azam FC ikazidi kujiwekea rekodi baada ya kuwa timu pekee ya Afrika Mashariki na Kati kupangwa kuanzia raundi ya kwanza tofauti na nyingine ambazo huanzia raundi ya chini kabisa ya awali.

Azam FC ikazidi kufanya maajabu baada ya kuiadhibu mabao 3-0 Bidvest Wits ya Afrika Kusini ugenini jijini Johannesburg, shukrani kwa mabao ya nahodha kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, beki Shomari Kapombe na nahodha Bocco, aliyepigilia msumari wa mwisho.

Kama kawaida Azam FC ikaendeleza rekodi yake ya ushindi wa asilimia 100 kwenye uwanja wake wa nyumbani katika michuano ya Afrika baada ya kuwabugiza mabao 4-3 timu hiyo na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 7-3 na kupangiwa kukutana na moja ya vigogo wa Afrika, Esperance ya Tunisia.

Mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Kipre Tchetche, aliyeuzwa nchini Oman mwanzoni mwa msimu huu, naye katika mechi ya pili dhidi ya Bidvest Wits, alifikia rekodi ya Mcha ya kufunga ‘hat trick’ kwenye michuano hiyo na kuwa mchezaji wa pili wa timu hiyo kuweza kufanya hivyo.

Licha ya Azam FC kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2, lakini iliweza kulinda heshima ya uwanja wake wa nyumbani baada ya kuichapa 2-1 nyumbani na kukubali kipigo cha 3-0 ugenini.

Hadi sasa kwa mujibu wa takwimu za mechi hizotokea walipoanza kuutumia uwanja wa  Azam Complex kwa michezo ya Kimataifa, Azam FC imefanikiwa kucheza jumla ya mechi sita nyumbani na kushinda zote bila kupoteza wala kutoa suluhu hata mchezo mmoja.

Mwaka 2017 (Kombe la Shirikisho)

Kama ilivyokuwa miaka mingine miwili iliyopita, mwaka huu pia Azam FC itakuwa moja ya timu iliyo kwenye mchuano mkali kuwania kuingia kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho, ikiwa imepangwa tena kuanzia raundi ya kwanza ikichuana na Mbabane Swallows Jumapili hii na ya marudiano ugenini Machi 19.

Azam FC ikivuka mtihani huo kwa kuwatoa Waswaziland hao itaingia kwenye hatua ya mwisho ya mtoano ‘play off’, ambayo itakutanishwa na moja ya timu kati ya 16 zilizotolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ikipenya tena hapo itaingia moja kwa moja katika makundi.

Mabingwa hao wanaingia katika michuano hiyo, wakiwa kwenye mwenendo mzuri tokea mwaka huu uanze ambapo katika mechi 15 ilizocheza haijapoteza mchezo wowote na ikiwa na safu ngumu ya ulinzi baada ya kuruhusu kufungwa bao moja tu.

Katika mechi saba zilizopita za ligi, Azam FC imeonyesha na kudhihirisha ubora iliyokuwa nao msimu huu baada ya kushuhudiwa ikimaliza kucheza dakika zote 630 bila kuruhusu wavu wake kuguswa, ikiwa imeshinda mechi tano na kutoka suluhu mbili.