WAKATI kikosi cha Azam FC kikiwa tayari kimeanza rasmi maandalizi kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mbabane Swallows Jumapili hii, habari njema kwa mashabiki wa soka nchini ni kuwa tayari viingilio vimewekwa hadharani mchana huu.

Mchezo huo wa awali wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo utafanyika katika Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 1.15 usiku, ambapo viingilio vilivyotangazwa ni vya aina tatu tofauti ambavyo vimezingatia makundi ya watu tofauti.

Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffary Idd, ameuambia mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa kiingilio cha chini kitakuwa ni Sh. 3,000 kwa mashabiki wa majukwaa ya mzunguko, V.I.P B vitakuwa ni Sh. 5,000 huku wale wa V.I.P A wakilipia Sh. 10,000 tu.

Idd amesema kwa kuwajali mashabiki, tiketi hizo zitaanza kuuzwa kesho Jumatano huku akifafanua ya kuwa na zitakuwa kwa mfumo wa elektroniki na mashabiki wataweza kuzinunua kupitia mtandao wa Kampuni ya Selcom, ambao ndio mawakala wa kuuza tiketi hizo.

Alisema wameamua kuuza tiketi hizo mapema, ili kuwarahisishia mashabiki wa soka nchini kupata tiketi hizo kwa haraka na kutosumbuka watakapokuwa wamefunga safari yao kuja kushuhudia mchezo huo.

“Kama unavyojua uwanja wetu ni mdogo, hivyo kwa kuuza tiketi hizo kwa mfumo huo tutakuwa tumewapunguzia usumbufu mashabiki wa soka kwani idadi kamili ikishatimia ya mashabiki wanaotakiwa basi zoezi la uuzaji tiketi litahitimishwa,” alisema.

Aidha alitoa wito kwa mashabiki kununua tiketi zao mapema ili kujiwekea uhakika wa kushuhudia uhondo wa mchezo huo kwani hadi sasa watu wengi wamekuwa na shauku kubwa ya kujitokeza uwanjani.

Katika hatua nyingine, waamuzi watakaochezesha mchezo huo kutoka nchini Benin wanatarajiwa kuwasili nchini Ijumaa hii, ambao ni Mwamuzi wa Kati Adissa Abdul Raphiou Ligali, Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Medegnonwa Romains Agbodjogbe huku Msaidizi Namba Mbili akiwa ni Babadjide Bienvenu Dina. 

Kikosi cha Azam FC, kinachodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola burudani kwa koo lako na Benki bora kabisa nchini ya NMB, kipo kwenye hali nzuri kuelekea mchezo huo kikiwa hakika majeruhi hata mmoja jambo ambalo linatia matumaini makubwa ya timu hiyo kupata matokeo mazuri.

Jambo pekee ambalo limebakia hivi sasa, ni mashabiki wa soka kwa ujumla wenu nchini hasa jijini Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti Azam FC kwenye mchezo huo kwani ndio moja ya timu pamoja na Yanga, ambazo zinaiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Afrika.