KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imepangiwa kucheza na Ndanda katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, utapangiwa tarehe hapo baadaye kutokana na Azam FC kuwa kwenye ratiba kali ya ushiriki wa Kombe la Shirikisho Afrika (CC), Jumapili hii itakipiga na Mbabane Swallows kabla ya kurudiana nayo ugenini Machi 19 katika wikiendi ya mechi za FA Cup nchini.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi burudani kwa koo lako cha Azam Cola na Benki bora kabisa nchini ya NMB, ilitinga hatua hiyo ya nane bora baada ya kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0 lililifungwa na winga anayekuja kwa kasi Ramadhan Singano ‘Messi’.

Kabla ya kucheza na Mtibwa Sugar, mabingwa hao Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu waliianza michuano hiyo kwa kuipiga Cosmo Politan mabao 3-1, ukiwa ni mchezo pekee ndani ya mechi 15 ambazo Azam FC imecheza mwaka huu na kuruhusu wavu wake kuguswa.

Ndanda nayo iliitupa nje The Might Elephant ya mkoani Ruvuma kwa jumla ya mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia suluhu ndani ya muda wa kawaida wa dakika 90 za mchezo, uliofanyika Uwanja wa Majimaji, mjini Songea.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana kwenye michuano hiyo, ambapo mara mwisho kukutana Ligi Kuu, Azam FC ilishinda bao 1-0 huku ule wa kwanza Ndanda ikipata ushindi wa 2-1.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotolewa jana, inaonyesha kuwa Simba amepangiwa kucheza na Madini, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha Machi 18 mwaka huu, huku siku kama hiyo Kagera Sugar ikiialika Mbao ndani ya Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

Mechi nyingine ambayo nayo haijapangiwa tarehe kutokana na ushiriki wa Yanga kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, itakuwa ni kati Tanzania Prisons watakaokuwa ugenini kukipiga na mshindi wa mchezo wa kiporo wa hatua ya 16 bora kati ya Yanga na Kiluvya United, utakaopigwa leo Jumanne ndani ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshindi wa michuano hiyo kikanuni anatarajia kujishindia kombe pamoja na kitita cha Sh. milioni 50 na kuiwakilisha Tanzania Bara kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.