BAADA ya kuichapa Stand United mabao 2-0 usiku wa kuamkia leo, sasa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imehamishia vita yake katika mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland.

Mchezo huo wa awali wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo, utafanyika ndani ya Uwanja wa Azam Complex Jumapili ijayo Machi 12 kabla ya kurudiana jijini Mbabane, Swaziland katika Uwanja wa Taifa wa Somhlolo Machi 19.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa timu hiyo, Aristica Cioaba, alisema kuwa mchezo huo ni muhimu sana kwao na kwa sasa wametilia mkazo kuandaa programu ya kupata matokeo mazuri dhidi ya Mbabane.

“Kila mmoja anafuraha baada ya kushinda mechi hii (Stand United), wakati wa maandalizi niliongea na kila mmoja kuwa nataka matokeo kwenye mchezo huo, umeona dakika 45 za kipindi cha kwanza kulikuwa kuna udhaifu kwenye pasi, lakini kipindi cha pili niliongea kwenye kikao na kila akaelewa na kupata matokeo,” alisema.

Cioaba, 45, alisema kuwa kuanzia wiki ijayo anataka kumuona kila mchezaji wake akiwa tayari kuelekea kwenye mchezo huo dhidi ya Mbabane, ambayo inakutana na Azam FC baada ya kuitoa Orapa United ya Botswana kwa jumla ya mikwaju ya penalti 3-2 kufuatia sare ya bao 1-1.

“Kuelekea mchezo huo ninamatatizo madogo kikosini, najua mashabiki kuna baadhi ya wachezaji hawakuwaona uwanjani dhidi ya Stand United, lakini hakuna tatizo lolote kubwa, niliwapumzisha baadhi ya wachezaji na naamini wachezaji wangu wote watakuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana aliyeiongoza kushika nafasi ya pili kwenye msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Ghana, alichukua fursa hiyo pia kutoa ujumbe maaalum kwa mashabiki wa Azam FC, ambapo amewaambia kuwa wanatakiwa kujitokeza kwa wingi Jumapili ijayo ili kuwasapoti wachezaji na kuwapa nguvu ya kuibuka na ushindi.

“Nilizungumza hili siku nne zilizopita, niliwapa ujumbe wangu mashabiki na watu wa hapa Tanzania, hivi sasa Azam FC inaenda kucheza mchezo muhimu wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya timu kutoka Swaziland (Mbabane Swallows), nadhani watu wengi wanatakiwa kutusapoti kwenye mechi hii ambayo si tu tunaiwakilisha Azam FC bali pia na Tanzania kwa ujumla.

“Watu wengi wanatakiwa kujitokeza na naamini mashabiki watakuja na kwa pamoja mashabiki, wafanyakazi, wachezaji, uongozi na kila mmoja wote wakikaa kwa malengo, lazima itatarajiwa mechi nzuri na matokea mazuri,” alisema.

Kocha huyo raia wa Romania, akiwa pamoja na wasaidizi wake Idd Nassor Cheche na Idd Abubakar waliofanikiwa kuijenga vema Azam FC ikiwa haijapoteza mchezo wowote tokea mwaka huu uanze, alimalizia kwa kuwaahidi mashabiki wa timu hiyo mchezo mzuri pamoja na matokeo mazuri.

“Ninachowahidi mashabiki wa Azam FC itakuwa ni moja ya mechi nzuri, kila mchezaji analitambua hilo kuhusu mechi hii na kwa uhakika wataingia uwanjani kucheza vizuri na kupata matokeo mazuri, ninaiamini timu yangu kuelekea mchezo huo,” alisema.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi ya aina yake ya kucheza jumla ya mechi 15 mfululizo mwaka huu bila kupoteza hata moja huku ikiwa imeruhusu wavu wake kuguswa mara moja tu.

Kama hiyo haitoshi ushindi uliopata jana dhidi ya Stand United, umeifanya Azam FC kujiongezea rekodi yake ya kucheza mechi saba mfululizo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) bila kuruhusu bao lolote kwa wavu wake.