HAISHIKIKI! Hivyo ndivyo unavyoweza kuuelezea mwenendo wa Azam FC, ambapo usiku huu imeendeleza kasi yake nzuri ya kuvuna pointi baada ya kuichapa Stand United mabao 2-0, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kuzidi kuzisogelea timu zilizo juu yake baada ya kufikisha jumla ya pointi 44 katika nafasi ya tatu, ikizidiwa pointi 11 na Simba iliyo kileleni kwa pointi 55 huku Yanga ikiwa nafasi ya pili kwa pointi zake 52 lakini ina mchezo mmoja mkononi.

Azam FC ililazimika kusubiri hadi dakika 45 za kipindi cha pili kuweza kuandikisha ushindi huo, ikianza kupata la kwanza dakika ya 58 kupitia kwa kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, aliyepiga shuti kali umbali wa mita 25, lililomshinda kipa wa Stand United, Frank Muhonge.

Hilo ni bao la pili kwa Sure Boy kwenye mchezo wa pili mfululizo wa ligi, la kwanza akifunga kwa shuti la aina hiyo hiyo nje ya eneo la 18 wikiendi iliyopita wakati Azam FC ilipoichapa Mwadui 2-0.

Alikuwa ni beki kisiki, Yakubu Mohammed, aliyeihakikishia ushindi Azam FC baada ya kuipatia bao la pili akimalizia kwa shuti kazi nzuri iliyofanywa na winga Ramadhan Singano ‘Messi’, aliyempigia krosi safi na kisha mfungaji kumpoteza maboya kipa wa Stand United.

Kwa hakika kupatikana kwa mabao yote hayo kulichangiwa na mabadiliko ya kiufundi, yaliyofanywa na Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, dakika ya 26 baada ya kumtoa Mudathir Yahya na kuingia winga Joseph Mahundi, ambaye alikuwa mwiba mkali kwenye safu ya ulinzi ya Stand United, ambayo mara kwa mara ilikuwa ikimafanyia rafu za makusudi hali iliyomfanya kutolewa dakika ya 81 na kuingia Shaaban Idd kufuatia kuumia.

Kama mshambuliaji wa Azam FC, Yahaya Mohammed, angekuwa makini kwenye mchezo huo angeweza kuipatia zaidi ya mabao matatu timu hiyo, lakini alikosa umakini na kujikuta akipoteza nafasi nyingi.

Rekodi ya Azam FC yazidi kupaa

Ushindi wa leo unaifanya Azam FC kuendeleza rekodi yake ya kutofungwa bao lolote kwenye mechi saba mfululizo za ligi hiyo (sawa na dakika 630), huku ikiwa haijapoteza mchezo wowote kwenye mechi 15 ilizocheza mwaka huu.

Baada ya kumalizika mcjhezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza tena mazoezi Jumatatu ijayo kujiandaa na mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika (CC) dhidi ya Mbabane Swallows, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumapili ijayo.

Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Himid Mao (C), Salum Abubakar, Frank Domayo/Abdallah Kheri dk 77, Yahaya Mohammed, Mudathir Yahya/Joseph Mahundi dk 26/Shaaban Idd dk 81, Ramadhan Singano