WAKATI kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kikitarajia kushuka dimbani kesho Jumamosi saa 1.00 usiku kuvaana na Stand United, kipa wa timu hiyo Aishi Manula, ameweka bonge la rekodi miongoni mwa makipa wote wanaoshiriki kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Rekodi hiyo anayoshikilia Manula ni ile ya kucheza mechi sita mfululizo za ligi (sawa na dakika 540) bila kuruhusu wavu wake kuguswa (clean sheet), tokea kuanza kwa mzunguko pili wa ligi hiyo unaoelekea raundi ya mechi za 24 wikiendi hii.

Tokea kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi, Azam FC imecheza jumla ya mechi nane, kati ya hizo Manula ameruhusu wavu wake kuguswa mara moja tu wakati timu hiyo ikivaana na Majimaji mkoani Songea kwenye sare ya bao 1-1.

Katika kudhihirisha uwezo wake langoni, tokea afungwe bao hilo mpaka sasa hajaruhusu tena bao lolote kwenye mechi sita za ligi zilizofuatia na kumfanya kuwa kipa pekee aliyefanya hivyo hivi sasa.

Manula ambaye pia ni miongoni mwa makipa tegemeo wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, katika mechi hizo nane za mzunguko wa pili ameiongoza Azam FC kutopoteza mchezo wowote, ikijizolea pointi 16 kati ya 24, zilizotokana na ushindi mara nne na sare nne.

Ubora huo wa Manula ambaye ana wastani wa kuokoa michomo saba hadi nane kwenye mechi moja, kwa kiasi kikubwa umeboreshwa na Kocha wa Makipa wa timu hiyo, Idd Abubakar, anayefanya kazi kubwa ya kuwapika makipa wa timu hiyo wakiwemo wengine wa timu ya vijana.

Mbali na Kocha huyo, pia safu kali ya ulinzi iliyotengenezwa hivi sasa ndani ya timu hiyo, ikiundwa na mabeki hodari Aggrey Morris, Yakubu Mohammed katika eneo la katikati la ulinzi pamoja na wale wa pembeni Shomari Kapombe, Bruce Kangwa, ambao wamekuwa wakisaidiana na Gadiel Michale na mkongwe Erasto Nyoni.

Vilevile Manula na safu yake ya ulinzi, wamekuwa wakipata ulinzi imara kutoka kwa viungo wa ukabaji, ambapo kwa mara kadhaa nahodha Msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, Frank Domayo, wamekuwa wakishirikiana vema pamoja na kiungo aliyekuwa majeruhi, Stephan Kingue.

Aishi azungumzia rekodi hiyo

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz leo kuhusu rekodi hiyo, Manula alisema ni jambo zuri kwao kama timu kuweza kucheza mechi sita bila kuruhusu bao huku akidai kuwa wao kama idara ya ulinzi wanajivunia kiujumla mafanikio hayo.

“Nadhani mabadiliko pia yamechangia, mabadiliko makubwa ambayo tumeyafanya kama sehemu ya ulinzi, raundi ya kwanza tulikuwa na wastani mbaya katika kuruhusu mabao, lakini pia tumeweza kurekebisha hilo na watu tumeweza kuimarika zaidi, tumeweza kuelewana na kufanya vizuri katika raundi hii ya pili, kwa ujumla tumecheza mechi nane, katika mechi hizo tumeruhusu bao moja tu ni kitu kizuri kwa kweli,” alisema.

Kipa huyo bora wa msimu uliopita kwenye mashindano yote (Ligi Kuu na Kombe la FA), alisema kuwa raundi ya kwanza hawakuwa imara kama ambavyo wako hivi sasa huku akiamini kuwa kipindi kigumu ilichokuwa imepitia Azam FC katika raundi hiyo, ilikuwa ni kipindi cha mpito tu na sasa wameimarika zaidi na kufanya vizuri.

Mbali na kufanya makubwa hayo kwenye ligi, itakumbukwa ya kuwa Manula alisimama vema kwenye milingoti mitatu ya goli kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi mwanzoni mwa mwaka huu na kuiongoza Azam FC kutwaa taji hilo bila kuruhusu wavu wake kuguswa na pia kutopoteza mchezo wowote.

Katika hatua nyingine, ameruhusu pia kufungwa bao moja tu kwenye mechi mbili za michuano ya Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup) inayoendelea, bao hilo likifungwa wakati Azam FC ikiichapa Cosmopolitan mabao 3-1 na timu hiyo kutinga hatua ya 16 bora ilipoipiga Mtibwa Sugar 1-0 na kusonga mbele kwa hatua ya robo fainali. 

Rekodi ya kiujumla ya kipa huyo msimu huu inaonyesha kuwa katika mechi 30 alizodaka za mashindano mbalimbali, amefanikiwa kutoka shujaa uwanjani kwa kutoruhusu bao (clean sheet) mara 18 huku akiruhusu wavu wake kutingishika mara 12 tu.

Azam FC ikiwa chini ya makocha bora kabisa walioiongoza timu hiyo kutopoteza mchezo hadi sasa tokeo mwaka huu uanze, Kocha Mkuu raia wa Romania, Aristica Cioaba, Msaidizi wake Idd Nassor Cheche na Kocha wa Makipa, Abubakar, kwa sasa ipo kwenye maandalizi ya mwisho kujiandaa na mtanange wa kesho dhidi ya Stand United utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 1.00 usiku.